Dodoma. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi pikipiki 10 zenye thamani ya Sh28 milioni kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuimarisha ulinzi na usalama kuelekea mbio za NBC Dodoma Marathon zitakazofanyika Julai 27, 2025.
Makabidhiano hayo yalifanyika leo Julai 24 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, yakihusisha pia utoaji wa jezi na vifaa maalum kwa washiriki wa mbio hizo. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Rosemary Senyamule pamoja na maofisa wa polisi na maafisa wa NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Serikali wa benki hiyo, Elvis Ndunguru.
Akizungumza katika hafla hiyo, Shekimweri ameishukuru NBC kwa mchango huo akisema umefika wakati muafaka kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu, ambapo mahitaji ya doria za kiusalama ni makubwa.
“Msaada huu wa pikipiki unatokana na ombi letu la mwaka jana, tunawashukuru NBC kwa kuitikia. Pikipiki hizi zitasaidia sana katika kuhakikisha usalama wa raia na mali, hasa katika kipindi hiki cha maandalizi ya marathon na uchaguzi,” amesema Shekimweri.
Aidha, alisifu maandalizi ya mbio hizo, akisema mwaka huu idadi ya washiriki imeongezeka kutoka 8,000 hadi 12,000 huku zawadi nazo zikiongezwa. Alitoa wito kwa wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kushiriki na kushangilia barabarani.

Kwa upande wake, Ndunguru amesema msaada huo ni sehemu ya uendelezaji wa ushirikiano kati ya NBC na Serikali, ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wa benki hiyo kwa jamii.
“Tumeitikia wito huu kama sehemu ya kushiriki kuhakikisha usalama wa washiriki wa mbio zetu na raia wote. Hili ni jiji letu na tukio hili limekuwa sehemu muhimu ya ajenda ya afya na maendeleo,” amesema.
Mbio hizo mwaka huu zinalenga kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, kusaidia wakunga kufikia 200 na kufadhili masomo ya wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Galus Hyera, Mrakibu wa Polisi, Daniel Bendarugaho amesema pikipiki hizo zitaongeza ufanisi wa doria na kusaidia kudhibiti uhalifu jijini humo.
“Zitatumika pia kuhakikisha usalama wa mbio za NBC Marathon, tukio kubwa lenye mvuto wa kitaifa,” amesema.
Mbio hizo zinatarajiwa kushirikisha wanariadha kutoka mikoa mbalimbali, zikiwa zimejikita pia katika kuibua utalii wa ndani na kuhamasisha huduma za afya na maendeleo ya jamii.