Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Rais Samia Suluhu Hassan atazindua reli ya kisasa ya mizigo (SGR) pamoja na kupokea mabehewa 70 yatakayotumiwa na reli ya zamani (MGR).
Mabehewa hayo yatajumuisha mapya 50 na mengine 20 yaliyofanyiwa ukarabati na yatatumiwa na reli ya zamani kufanya shughuli za usafirishaji wa mizigo.
Hayo yameelezwa leo Julai 25,2025 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa wakati akizungumzia katika hafla ya uzinduzi wa bandari ya Kwala jijini Dar es Salaam ambayo itaambatana na shughuli hizo zingine Julai 31,2025.
“Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa treni ya SGR alisema lengo kuu la treni ya mizigo ni kuongeza usafirishaji wa mizigo kutoka eneo moja kwenda eneo lingine na treni hii itakapofika Burundi na DRC Congo,” amesema
Profesa Mbarawa amesema reli hiyo ya mizigo ni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na tayari treni hiyo imekwisha fanyiwa majaribio Juni mwaka huu kwa kusafirisha tani 700 za mzigo kupitia kontena 10.
Pia amesema Julai mwaka huu, mzigo wenye uzito wa tani zaidi ya 1000 ulisafirishwa kupitia treni ya SGR kwa majaribio.
Ameongeza kuwa treni hiyo mabehewa yataongezwa hadi kufikia 30, lengo kuwezesha treni kufikia lengo la kubeba mizigo tani zaidi ya 200,000.
Akizungumzia bandari ya Kwala, Profesa Mbarawa amesema Serikali imeamua kujenga kwani hakuna fidia yeyote ambayo ilihitajika ili wananchi wapishe mradi husika pamoja na uwepo wa changamoto ya ufinyu wa nafasi za kushusha makontena katika bandari kavu.
Amesema Rais Samia atakapozindua bandari hiyo, faida mojawapo itakayoshuhudiwa ni ongezeko la mapato ya Serikali na kupunguzwa kwa gharama za usafirishaji wa mizigo.
“Kutakuwa na ongezeko la shehena zinazohudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam, shughuli za kiuchumi zitaimarika katika Jiji la Dar es Salaam hasa kwa kupunguzwa foleni,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Plasduce Mbomsa amesema kuzinduliwa kwa bandari ya Kwala haitakuwa sababu ya malori kuzuiliwa kuingia mjini.
Amesema bandari hiyo itasaidia kupunguza foleni ya malori katikati ya mji na ndio adhima kuu ya Serikali kuanzisha bandari hiyo kuchochea shughuli za maendeleo.
Bandari ya Kwala inatarajiwa kuhudumia kontena 823 kwa siku zikiwamo zinazokwenda nchi jirani ikiwa ni sawa na kontena 300,395 kwa mwaka sawa na asilimia 30 ya kontena zinazohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.