Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RC), Nurdin Babu ameitaka jamii kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuacha ngono zisizo salama na kutumia kinga ili kuepuka na au kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (HIV): ’’Kwani ugonjwa huu bado upo’’
RC Babu amesema hatua hiyo itaondoa unyanyapaa na kupunguza vifo kufikia mwaka 2030.
Mkuu huyo wa mkoa amesema hayo jana Alhamisi, Julai 24, 2025 wakati wa kukabidhi vyeti vya pongezi kwa mashujaa wa kampeni ya GGML Kili Challenge waliopanda Mlima Kilimanjaro kwa miguu na baiskeli.
Kampeni hiyo imefadhiliwa kwa pamoja na mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids)na wadau wengine kwa lengo la kukusanya fedha za kupambana na Virusi vya Ukimwi katika kufanikisha ajenda ya Tanzania bila Ukimwi inawezekana.
Kampeni hiyo inaunga mkono malengo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikia sifuri tatu ifikapo mwaka 2030, ambazo ni kuzuia maambukizi mapya ya VVU, vifo vinavyotokana na Ukimwi na unyanyapaa.
Pia, utekelezaji wa Dira 2050 unalenga kuongeza umri wa kuishi wa Watanzania kutoka wastani wa miaka 68 ya sasa hadi 75 kwa kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora na kushiriki ipasavyo katika ujenzi wa Taifa.
RC Babu katika maelezo yake amesema: ’’Kuweni makini na kuchukua tahadhari, ugonjwa wa Ukimwi bado upo.”
Amesema jamii likiwemo kundi kubwa la vijana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 30 linahitaji elimu zaidi kuhusu Virusi vya Ukimwi na jinsi ya kujikinga na kuwalinda wengine.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat amesema mgodi huo utaendelea kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya Virusi vya Ukimwi ili kufanikisha malengo ya sifuri tatu (yaani hakuna maambukizi, hakuna unyanyapaa, na hakuna vifo kufikia mwaka 2030).
“Mgodi wa GGML sio tu unajihusisha na uchimbaji madini wenye uwajibikaji, bali pia unachangia maendeleo ya jamii kupitia sekta mbalimbali, ikiwemo afya ambayo ni msingi mkuu wa maendeleo,” amesema.
Amesema upandaji wa Mlima Kilimanjaro haukuwa tu kielelezo cha utalii, bali ulikuwa kielezo cha uzalendo ambapo waliopanda mlima huo, wakiwemo watoto yatima wawili wenye umri wa miaka 13 walijitolea kwa jasho na maumivu kwa ajili ya kuonesha uzalendo huo na upendo kwa jamii.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Uendelevu na Mahusiano, Africa, AngloGold Ashanti, kampuni mama ya GGML, Simon Shayo amesema katika kuadhimisha miaka 25 ya mgodi huo hapa nchini, wanaona fahari kampeni hiyo ikiendelea kufanyika kila mwaka kwa kipindi cha miaka 23 mfululizo, kuendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali na kuleta matokeo chanya katika jamii.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kupitia kampeni hii katika miaka ijayo ili kufikia malengo yaliyowekwa,” amesema Shayo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa amesema mbali na upandaji wa Mlima Kilimanjaro, kampeni hiyo pia ilihusisha upimaji wa hiari wa UKIMWI na utoaji wa elimu ya kujikinga, ambapo jumla ya watu 1,632 walipimwa, nusu yao wakiwa wanawake, na kondomu 54,728 zilisambazwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed amesema mgodi huo umechangia miradi mbalimbali ya kijamii mkoani humo ikiwemo maji, ujenzi wa barabara na kulea kituo cha watoto yatima kama sehemu ya kuunga mikono juhudi za Serikali.