Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amewaongoza Watanzania kuadhimisha Siku ya Mashujaa.
Baada ya kuwasili katika Uwanja wa Mashujaa uliopo Mji wa Serikali Mtumba, mkoani Dodoma yalikofanyika maadhimisho hayo leo Julai 25, 2025 Rais Samia amepokewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda.
Kisha ilitolewa salamu ya heshima kwa Rais ikifuatiwa na wimbo wa Taifa la Tanzania na ule wa Afrika Mashariki.

Rais wa Samia Suluhu Hassan na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa katika uwanja wa Mashujaa Mtumba Jijini Dodoma Julai 25, 2025.
Hatua hiyo ilifuatiwa na kupigwa kwa ala ya ‘Last Post’ kwa kuweka silaha begani kisha likafuata gwaride la maombolezo kwa kupindua silaha chini.
Mizinga miwili ilipigwa ikifuatiwa na hali ya ukimya kwa dakika moja, baada ya hapo gwaride lilipiga saluti kwa maofisa na askari wenye sare.
Rais Samia aliweka mkuki na ngao kwenye mnara wa mashujaa ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka.
Baadaye Mkuu wa Majeshi aliweka sime na kisha mwakilishi wa mabalozi aliweka shada la maua wakifuatiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma aliyeweka shada na mwakilishi wa mashujaa wa Taifa akiweka shoka.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akishiriki maadhimisho ya Siku ya Mashujaa katika uwanja wa Mashujaa, Mtumba Jijini Dodoma leo Julai 25, 2025.
Baada ya shughuli hiyo, viongozi wa dini walitoa dua kuwaombea mashujaa, pia amani na utulivu wa Taifa.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo, Brigedia Jenerali Mndolwa amewataka waandishi wa habari nchini kuwa wazalendo ili amani iliyopo iendelee kudumu.

“Waandishi wa habari mnapoandika habari za mashujaa hawa muandike zinazowaheshimisha wao na Taifa, kuweni wazalendo maana nchi inatoka mbali, inahitaji msaada wa kila mtu ili tuendele kuwa na amani, maana nyingi zimebomoka,” amesema.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, mawaziri, makatibu wakuu, maofisa waandamizi wa Serikali, mabalozi na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Siku ya Mashujaa huadhimishwa kila Julai 25 kwa lengo la kuwakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliotoa mchango mkubwa katika historia ya Taifa.