Sh19.9 bilioni zatolewa ujenzi wa stendi mpya Babati

Babati. Serikali imetoa Sh19.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha mabasi katika eneo la Makatani mjini hapa mkoani Manyara.

Ujenzi wa kituo kipya cha mabasi utasababisha faraja kwa watu wa Babati, ambao kwa muda mrefu walitamani ujenzi mpya ili kuchochea uchumi wa eneo hilo.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amelieleza Mwananchi leo Julai 25 mwaka 2025 kwamba ujenzi huo utafanyia kwa miezi 15, hali itakayochechemua uchumi kwa wakazi wa mkoa huo na jirani.

Amesema Halmashauri ya Mji wa Babati ni miongoni mwa halmashauri 15, ambazo zimepata mradi kama huo wa ujenzi wa vituo vipya vya mabasi, kati ya halmashauri 184 nchini.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga akizungumza kwenye uzinduzi wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi kilichopo Makatanini mjini Babati. Picha na Joseph Lyimo

Amewataka wataalamu wa halmashauri hiyo wale wa wakala wa barabara za mjini na vijijini (Tarura) kuusimamia vizuri mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Sendiga ametumia fursa hiyo kumtaka mkandarasi kuwapa kipaumbele kwa kutoa ajira kwa wazawa wa eneo hilo hasa kwa kazi ambazo hazihitaji utaalamu.

Amewapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kupokea mradi huo, utakaohusisha barabara za lami zenye urefu wa kilomita 4.7 na mitaro ya kupitisha maji kilomita 8.15 katika maeneo mbalimbali ya mji wa Babati.

“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wa Manyara na ninawataka watu wote kuilinda miundombinu hii,” amesema Sendiga.

Mkurugenzi wa mji wa Babati, Shabaan Mpendu amesema ndani ya stendi hiyo kutajengwa jengo la utawala, maduka 60, vibanda 12 vya mama lishe, vibanda 16 vya tiketi, vitatu vya walinzi na kimoja cha kukusanyia taka.

“Vibanda vingine ni cha jenereta, vyoo, mnara wa tenki la maji na ujenzi wa barabara za lami za mitaa kilometa 4.7, mitaro ya kupitisha maji kilometa 8.15,” amesema Mpendu.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Wesons Engineers inayojenga mradi huo, Mugore Chambili amesema mradi huo wataumaliza kwa muda uliopangwa na kwa viwango vinavyotakiwa.

Mkazi wa mtaa wa Maisaka, Simon Bayo ameipongeza Serikali kwa kutenga fedha hizo kwani muda mrefu umepita bila hatua hiyo kuchukuliwa.