SIMBA inaripotiwa imemnasa beki wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Rushine De Reuck kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Mtandao wa idiskitimes.co.za wa Afrika Kusini umeripoti kwamba beki huyo mwenye umri wa miaka 29 anaondoka Mamelodi Sundowns baada ya kuitumikia kwa miaka minne.
Ndani ya Simba, De Reuck anategemewa kuziba pengo la Che Fondoh Malone ambaye ameachana na timu hiyo na kujiunga na USM Alger ya Algeria.
Inaripotiwa kwamba uhamisho wa Rushine De Reuck umetokana na pendekezo la Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.
Davids aliwahi kufanya kazi na De Reuck katika timu ya Maritzburg ya Afrika wakati huo akiwa Kocha Mkuu.
Nusu ya msimu uliopita, De Reuck aliitumia kwa kucheza kwa mkopo katika timu ya Maccabi Petah Tikva ya Israel ambayo ilimpa nafasi ya kucheza katika mechi nne tu.
Uhamisho wa De Reuck utamfanya awe mchezaji wa kwanza raia wa Afrika Kusini kuwahi kuichezea Simba lakini anakuwa wa pili kutoka taifa hilo kucheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ikumbukwe mchezaji wa kwanza wa Afrika Kusini kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara ni Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ ambaye aliwahi kuichezea Yanga katika msimu wa 2022/2023.
Rushine aliibukia katika kituo cha Soka cha ASD jijini Cape Town kisha akapata fursa ya kucheza kwa msimu mmoja katika timu ya Pacos Ferreira ya Ureno kuanzia 2014 hadi 2015 ambapo alijiunga na Hellenic.
Mwaka 2017 alijiunga na Maritzburg aliyoichezea hadi 2021 alipojiunga na Mamelodi Sundowns.
Mwaka 2021, De Reuck alifanikiwa kuibuka mshindi wa tuzo ya Beki Bora wa Ligi Kuu Afrika Kusini akiwa na jezi ya Maritzburg aliyoitumikia kwa zaidi ya mechi 77.
De Reuck amewahi kuichezea timu ya Taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ ambapo amepata nafasi kikosini katika michezo saba.