MABOSI wa Singida Black Stars wanaendelea kuvuta majembe ya msimu ujao, ikijapanga kumalizana na kiungo mshambuliaji wa Zoman FC, Idrissa Diomande ‘Yaya Toure’ kutoka Ivory Coast.
Rekodi zinaonyesha kiungo huyo ambaye ameichezea Zoman FC kwa miaka miwili, amemaliza kibabe msimu uliopita kwa kufunga mabao tisa na kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa klabu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, kiongozi wa klabu hiyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema, Singida imefanya maamuzi ya kusaka saini ya kiungo huyo kutokana na ubora wake.
“Ni kiungo mshambuliaji mzuri ambaye anajua kutengeneza nafasi, pia kufunga, amefanya vizuri akiwa Ligi ya Ivory Coast na tutakuwa naye kwa msimu ujao.
“Unapoona kiungo anafunga zaidi ya mabao manane utaona namba zinavyombeba, pia amekuwa mchezaji bora kwenye timu yake, tunataka aje kuchukua nafasi ya Tchakei ambaye tuna uwezekano wa kumuuza huko Uarabuni.
Marouf Tchakei ameitumikia Singida Black Stars misimu miwili akitokea Fountain Gate ambayo aliichezea mwaka mmoja akifunga mabao matano.
Kama Singida itamuuza Tchakei basi itakuwa imesalia na viungo washambuliaji watano, hivyo akiongezeka na Muivory Coast huyo watakuwa sita.