KAMA kweli Simba imemsajili Jonathan Sowah, basi watu wa mpira tunakubaliana imepata mshambuliaji ambaye analijua kweli goli na ni tishio kwa wapinzani.
Jamaa anajua kufunga, pia anaweza kukaa katika nafasi na kufanya vitu vingine vya kishambuliaji anapolikaribia lango la timu pinzani kama vile kupindua mabeki na kuwanyima uhuru.
Namba zake Ligi Kuu Bara msimu uliopita zinajieleza na ukizikataa utakuwa na roho ya kichawi tu maana alifunga mabao 13 katika mechi 13 za ligi, hivyo kuwa na wastani wa bao moja katika kila mchezo jambo ambalo hakuna aliyeweza kulifanya tofauti na yeye.
Sisi hapa kijiweni tulishakubaliana kitambo katika jambo la kisoka linaloamriwa na takwimu, hatuhitajiki kubishana sana na badala yake yule mwenye namba zinazojitosheleza ndiye kinara kama ilivyo kwa Sowah kwa kulinganisha na mechi alizocheza.
Kijiwe kinamkumbusha Sowah, timu anayoenda sasa siyo Singida Black Stars kwani ina kundi kubwa la mashabiki na mahitaji iliyonayo kwa kila mchezaji ni makubwa, hivyo anapaswa kuishi kwa weledi wa hali ya juu Simba.
Kwanza anatakiwa ahakikishe anajitahidi kuwa na nidhamu nzuri nje na ndani ya uwanja ili kuepuka adhabu zinazoweza kumfanya akosekane kwenye baadhi ya mechi za timu hiyo maana Simba inamsajili na siyo atazame mechi jukwaani kwa makosa ya kizembe.
Ni mchezaji ambaye anaonekana ana hasira za karibu sasa kwa timu kama Simba ambayo wachezaji wa timu pinzani huwa wanatumia hata mbinu za kuwatoa mchezoni wachezaji wake ili wafanye matukio ya utovu wa nidhamu yanayoweza kuwasababishia kadi.
Jambo lingine ni kuhakikisha anaonyesha kiwango bora na chenye muendelezo hasa kwenye mechi kubwa ili kutokaribisha hisia hasi kwa watu wa Simba juu yake na mahusiano aliyonayo na baadhi ya watu wa Yanga.
Ile kauli aliyotoa siku za nyuma anamchukulia Injinia Hersi ambaye ni Rais wa Yanga kama baba yake, inaweza kuwa fimbo ya kumchapia Simba ikiwa hatofanya vizuri