TMDA yatoa onyo kwa wamiliki wa maduka ya dawa, kuwalinda watumiaji

Njombe. Wamiliki wa maduka ya dawa baridi nyanda za juu kusini wametakiwa kuzingatia kikamilifu sheria, miongozo na taratibu za usambazaji na uuzaji ili kujiepusha na hasara ya kutaifishiwa bidhaa na kufutiwa leseni za maduka yao endapo watabainika kwenda kinyume.

Wakati huohuo imeelezwa kuwa ni hatari kuuza dawa za binadamu kuuzwa maeneo yasiyoruhusiwa kwani kunahatarisha afya za watuamiaji kutokana na matumizi holela na kutofuata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari wanaotambulika kisheria.

Hayo yamesemwa leo Julai 25,2025 na Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Anitha Mshighati, wakati akikabidhi msaada wa dawa zilizotaifishwa zenye thamani ya zaidi ya Sh.17milioni kwa zahanati za magereza na jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) zilizopo mkoani Njombe.

Amesema mamlaka hiyo haitosita kuchukua hatua za kisheria kwa wamiliki wa maduka ya dawa wasiofuta sheria ili kulinda afya za watumiaji wa dawa zinazouzwa kwenye maduka yao.

Amesema dawa zilizotolewa kwenye zahanati hizo ni sehemu ya shehena zilizokamatwa zikiuzwa kinyume cha sheria kwenye baadhi ya maduka ya dawa, na sasa zimeelekezwa kwenye taasisi zenye mahitaji ya haraka ya huduma za afya.

Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Anitha Mshighati akikabidhi msaada wa dawa kwa mkuu wa gereza la wilaya ya Njombe Jamhuri Njaidi katika hafla iliyofanyika huko wilayani Njombe.

Mshighati amesema TMDA itaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza ili kudhibiti uuzaji holela wa dawa usiozingatia usalama wa wananchi na kuhakikisha sheria, taratibu na miongozo inazingatiwa katika uuzaji wa dawa.

Amesema dawa zikitolewa katika maeneo ambayo siyo rasmi hata ushauri unaotolewa hauwezi kuwa wakajitosheleza kwa mgonjwa kwa sababu mtoaji wa dawa hizo wakati mwingine hana elimu ya kutosha juu ya matumizi yake hivyo kumuathiri mtumiaji.

“Sasa kama dawa haipo sehemu sahihi maana yake itatolewa kiholela jambo ambalo ni hatari. Mfano antibayotiki zikitolewa kiholela zitaleta madhara na usugu kwa mtumiaji na baadaye kushindwa kutibika tena kwa dawa ya aina hiyo,” amesema Mshighati.

Amewataka wananchi kuchukua au kununua dawa sehemu sahihi au katika maeneo rasmi yaliyoruhusiwa ili kuepuka kupata madhara yanayoweza kuwapata kwa kutumia dawa kiholela.

Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Njombe, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Jamhuri Njaidi, ameishukuru TMDA kwa msaada huo, akisema umekuja wakati muafaka na utaongeza upatikanaji wa dawa kwa mahabusu na wafungwa kwani huduma za afya ni haki ya msingi kwa kila mtu, bila kujali mazingira ya kifungo.

Ameitaka jamii kufanya matendo ya huruma kwa kutoa kwa wenye uhitaji wakiwemo wafungwa magerezani pamoja na maeneo mengine ambayo kuna uhitaji wa vitu mbalimbali.

“Wengi wao maeneo kama haya jamii inaogopa sana wanajua wakifika ni changamoto lakini sisi tunawakaribisha sana tupo tayari kupokea misaada siyo tu madawa mambo yapo mengi,” amesema Njaidi.

Mganga Mfawidhi Zahanati ya Magereza Wilaya ya Njombe, Ramadhani Idd Bakari amesema msaada huo wa madawa utawasaidia kwani uhitaji ni mkubwa na kila siku wanapokea wagonjwa kuanzia kumi hadi kumi na tano.

Amesema magonjwa yanayoongoza kupatiwa huduma katika zahanati hiyo ni magonjwa ya njia ya hewa kutokana na hali ya hewa ya mkoa huo ikiwemo magonjwa ya kifua pamoja na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo presha na kisukari.

“Niwaase jamii kuboresha taratibu zao za maisha ili kuepuka magonjwa haya ikiwemo kufanya mazoezi mara kwa mara,” amesema Bakari.

Mmoja ya wauzaji wa dawa za binadamu mkoani Njombe, Raphael Nsumba, amesema sababu kubwa ya watu wa maduka ya dawa kuweka  dawa au kuuza dawa ambazo haziruhusiwi kuwepo kwenye maduka hayo ni za kibiashara.

“Tahadhari kubwa naweza kusema ni usugu wa dawa hasa dawa za bakteria ambazo hizi zikitumiwa vibaya kwa mfano matumizi ya nusu dozi yanapelekea usugu wa dawa na maduka madogo ya dawa ndipo ambako watu wanaweza kuzipata nusu dozi kwa urahisi,” amesema Nsumba.