Visa, mikasa wanaotoswa stendi ya Magufuli, mikoa minne yaongoza

Dar es Salaam. Kwa wale ambao si wazaliwa wa Jiji la Dar es Salaam, kila mmoja ana simulizi yake ya namna alivyopokewa na mwenyeji wake alipofika ndani ya jiji hilo kwa mara ya kwanza.

Wapo wanaoeleza namna bodaboda walivyotumwa kuwapokea, wengine walifuatwa stendi na kupokewa kwa bashasha na wenyeji wao, lakini pia kuna waliotelekezwa stendi na kulazimika kuomba msaada kurudi walikotoka.

Si hivyo tu, wapo walioamua kujichanganya mtaani kuanza maisha mapya baada ya kutelekezwa.

Inaelezwa katika stendi kuu ya mabasi Magufuli, iliyopo Mbezi Luis jijini humo, baadhi ya wageni kutoka mikoa mbalimbali hufikwa na kadhia ya ama kutelekezwa au kuwakosa wenyeji wao.

Mkuu wa Idara ya Habari na Matangazo wa stendi hiyo, Majaliwa Shikilla anasema wapo wageni wanaokosa wenyeji, ambao wengine hulazimika kukaa stendi hadi siku tatu wakisubiri kuona kama watafuatwa.

“Sina takwimu kamili, lakini kila siku hapa stendi kuna wageni wanaowasili kutoka mikoa mbalimbali na kufikwa na changamoto ya kuwakosa wenyeji wao,” amesema Majaliwa.

Amesema mikoa inayoongoza kwa wageni kukosa wenyeji wanapowasili stendi ni Kigoma, Tabora, Geita na Kagera.

“Kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma na mingine si kama hawapo wanaokosa wenyeji, huko pia wapo lakini si kwa kiwango kikubwa kama wale wanaofika hapa kutoka kwenye mikoa hiyo minne niliyoitaja,” amesema.

Anasema pia wapo wenyeji ambao hupotezana na wageni wao, hivyo nao hufika idara hiyo kutoa taarifa ambayo baada ya kuipokea humtangaza mgeni anayetafutwa kwa jina lake, mkoa alikotokea na basi alilokuwa amepanda ili kukutanishwa na mwenyeji wake.

“Changamoto huwa kwa wageni ambao wamekosa mawasiliano ya wenyeji, wakiletwa ofisini tunachukua taarifa zao na kuwaelekeza wakae eneo la kupumzikia abiria, wapo ambao humaliza hadi saa 24 bila mwenyeji kufika,” anasema na kuongeza:

“Wapo wanaofikisha hadi siku tatu bila kumpata mwenyeji wake, hawa ni wale wanaoambiwa ‘njoo Dar maisha ni mazuri’, anapanda basi anakuja au wale wanaopakizwa kwenye basi kuja kufanya kazi za ndani, wakifika mwenyeji hapatikani kwenye simu,” amesema.

Amesema, “wanaowasafirisha kutoka mikoani wakati mwingine hawawapi mawasiliano, wapo wanaoambiwa nenda tu utapokewa Mbezi Magufuli ukifika, au wengine wanaambiwa ‘nenda namba hii hapa, ukifika utaomba simu upige’,” anasema.

Majaliwa anasema: “Wengi huwa mabinti wa kazi za ndani kati ya miaka 15 na 18. Akifika stendi kila mtu yupo ‘bize’ hakuna wa kumpokea anakaa tu stendi. Nishauri unapomsafirisha mtu huyu, hajawahi kufika Dar ni bora umkabidhi kwa kondakta na mwenyeji awepo stendi muda basi linawasili.”

Kwa wanaokosa wenyeji kwa muda mrefu, anasema idara hiyo huwapeleka ofisi ya utawala ili kupata msaada wa kurejeshwa walikotoka.

“Mgeni wa aina hii kama amekosa kabisa mawasiliano na mwenyeji wake na hana ndugu, ataandikiwa barua ili kupata msaada wa kusafirishwa. Wale wenye mawasiliano na ndugu zao kule walikotoka watapigiwa simu ili wamtumie nauli arudi,” anasema na kuongeza:

“Ila wapo wengine akishafika Dar na kuona ametelekezwa anaamua kutorudi alikotoka, wengine wanaamua tu kujichanganya na kuingia mtaani.”

Shuhuda za waliotelekezwa

Majebere Marando anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30, anakumbuka alivyomkosa mwenyeji wake baada ya kufika Dar es Salaam na kulazimika kulala stendi kwa siku mbili.

Anasema alipewa ‘mchongo’ wa kuja Dar es Salaam na rafiki yake wa utotoni ambaye walizaliwa kijiji kimoja mkoani Kigoma.

“Alipokuwa akija likizo na kutuletea zawadi niliamini Dar maisha ni rahisi, nikamuomba na mimi nije anitafutie kibarua akakubali na akanipa mawasiliano yake, nilifanya vibarua vya kulima nikapata nauli,” anasimulia.

Marando anasema: “Niliondoka kijijini nikiwa na matumaini ya kufikia na kusaidiwa naye ili nami niwe na maisha bora, lakini ilikuwa tofauti, kaka yangu yule alinitelekeza stendi.”

Anasema alikaa stendi kwa siku mbili kabla ya kuamua kujichanganya na vijana wengine mtaani kufanya vibarua kwa kuwa hakuweza kurudi tena kijijini.

Marando anasema alianza kupiga debe katika stendi hiyo ambako pia alilala.

Baada ya miezi sita anasema alipata mtaji akapanga chumba kwa gharama ya Sh15, 000 kwa mwezi eneo la Luguruni, ambacho hakikuwa na umeme wala maji. Kisha akaanzisha biashara ya kuchoma mahindi anayoendelea nayo hadi sasa.

“Nilianza na mtaji wa Sh30, 000, nilinunua jiko, wavu na mahindi ya Sh10,000 nikaanza biashara,” anasema.

Kwa biashara hiyo anasema hivi sasa ana uhakika wa kuuza na kupata Sh50,000 kwa siku katika kijiwe chake kilichopo Kibamba.

“Nusu ya pesa hiyo ni faida, ndivyo nilianza maisha, yule mwenyeji wangu sikumtafuta tena,” anasema.

Kwa upande wake, Nasra Omary (18) anasema miaka mitatu iliyopita alifika Dar es Salaam akitokea Iringa na alipofika stendi hakumkuta mwenyeji wake.

“Niliambiwa mwenyeji nitamkuta stendi, nilipewa kikaratasi chenye namba yake, nilipokuwa kwenye basi niliomba simu nipige haikupatikana hadi tumefika Dar, sikuwa na pa kwenda nikaanza kulia. Kuna mama alinichukua palepale stendi mpaka sasa naishi kwake nikimsaidia kazi za ndani,” anasema.

Nasra anayeishi Mwenge, anasema anafurahia maisha ya Dar es Salaam na bosi wake aliyempa kazi anayeishi naye mwaka wa tatu sasa.

“Mwanzoni alianza kunilipa mshahara Sh50, 000 akaniongezea hadi Sh80,000, sikuwahi kumfahamu mwenyeji ambaye alitakiwa anipokee nilipotoka Iringa. Hata hivyo, dada (bosi wake) alikwenda na mimi nyumbani Iringa kupajua kwetu baada ya kuishi kwake kama miezi mitatu,” anasema.

Kati ya watu 20 waliozungumza na Mwananchi wakieleza namna walivyopokewa na wenyeji wao walipofika Dar es Salaam kwa mara ya kwanza, 15 wamesema walipewa maelekezo ya kuchukua bodaboda baada ya kufika stendi.

Wawili wameeleza jinsi walivyotelekezwa stendi bila kujua waende wapi, huku watatu kati yao ndiyo waliowakuta wenyeji wao wakiwasubiri stendi.

Denis Naftari ni miongoni mwa waliopokewa, anasema alimkuta kaka yake mkubwa stendi ya Ubungo akimsubiri.

Licha ya kupokewa, anasema walipofika nyumbani alishangazwa na maisha ya ndugu yake huyo, kwani kwa siku tatu ilikuwa hakuna stori za hapa na pale zaidi ya salamu, maisha ambayo aliyazoea baada ya miezi kadhaa.

Hellena Mutafungwa yeye anasema aliposhuka aliambiwa achukue pikipiki kisha ampe simu dereva ili aelekezwe ni wapi anatakiwa kufika.

“Nilikuwa nakwenda kwa baba mkubwa, mara zote alipokuja kijijini familia nzima tulikwenda stendi kumpokea, lakini kwake ilikuwa ni tofauti. Hili lilinishangaza lakini baada ya kuishi kwa muda Dar es Salaam, nimeona ni jambo la kawaida,” anasema.

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam waliozungumza na Mwananchi wamesema mazingira ya jiji ndiyo yanayosababisha kuonekana watu wapo ‘bize’ tofauti na miji mingine.

Mwanasaikolojia na mchambuzi wa masuala ya kijamii, Deogratius Sukambi anasema tofauti ya maisha ya Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, yanachangiwa na hali ya kiuchumi na miundombinu.

“Kutoka Tabata kwenda Mbezi Luis kunahitaji saa za kutosha ili kufika, hivyo anapokuja mgeni, wengine huona kuliko kwenda kumpokea ni rahisi zaidi achukue pikipiki, kunapunguza gharama pia. Hili ni suala la social setting (mazingira ya kijamii yanayoathiri jinsi watu wanavyotenda), pia kuna mgongano wa kitamaduni,” anasema.

Mbali na hilo, anasema: “Dar es Salaam wenye mji wao hawapo, hivyo tunapokutana mjini kila mmoja ana utamaduni wake hatuishi kwenye tamaduni hizo.”

Amesema matumizi ya teknolojia pia ni makubwa, kwamba watu wamezoea ku-chat hivyo wanakuwa na uvivu wa kutembeleana.

“Lakini si kama watu wengine wana upendo kuliko wa Dar es Salaam, hapana,” amesema.