Dar es Salaam. Mzazi unafahamu mtoto wako ananunua nini katika ile fedha unayompatia kila siku anapokwenda shule?
Kwa kawaida watoto hupendelea kununua vitafunwa vyenye sukari nyingi, vinywaji kama juisi, soda, biskuti na vinginevyo, huku kinywaji cha kuongeza nguvu maarufu ‘energy drink’ kikiwa nacho kinapendelewa zaidi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya ‘Utafiti wa Afya, Viashiria na Malaria’ ya mwaka 2022, watoto wenye umri kati ya miezi sita hadi 23, wapo hatarini kupata ugonjwa wa kisukari, kutokana na mtindo mbovu wa maisha na vinywaji wanavyotumia.
Ripoti hiyo iliyofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imeonesha kundi hilo lipo hatarini kwa sasa kupata kisukari na kuongeza uzito uliopitiliza.
“Asilimia 30 ya watoto wenye umri wa miezi sita hadi 23 wanalishwa vinywaji vyenye sukari huku asilimia tisa ya watoto wenye umri huo wakilishwa vyakula visivyo na virutubisho muhimu,” imesema ripoti hiyo.
Takwimu hizo ni sawa na watoto watatu kati ya 10 ambao wapo hatarini kupata magonjwa ya kisukari na moyo, kutokana na aina ya vinywaji wanavyotumia katika umri huo.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini vyakula na vinywaji hivyo hatari kwa afya za watoto, vikiuzwa kiholela katika maeneo ya kuzunguka shule za msingi na sekondari.
Wakati kasoro hiyo ikionekana, imebainika hali hiyo inachangiwa na wazazi hasa maeneo ya mijini kutotoa ushirikiano katika kutekeleza mwongozo wa chakula shuleni, unaotaka wachangie gharama ya kuwapa chakula. Badala yake huwapa fedha wanafunzi wakajinunulie vyakula wanavyohitaji ili kupunguza njaa wawapo shuleni.
Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la vyakula vya watoto vyenye sukari ya kuongezwa viwandani zikiwemo juisi na vyakula vingine vya namna hiyo, vikiuzwa kiholela maeneo ya kuzunguka shule.
Juisi hizo ambazo hutengenezwa kwa kemikali nyingi, zinatajwa kuwa na athari kiafya kwa mujibu wa matokeo ya utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani, yaliyoonyesha watoto wanaokunywa vinywaji hivyo wapo kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa pumu.
Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha magonjwa 10 yaliyoongoza kwa watoto chini ya miaka 5 mwaka 2023 ni maambukizi katika mfumo wa hewa wa juu, mfano mafua na kikohozi ambapo watoto milioni 5.41 waliumwa sawa na asilimia 38.8 huku homa ya mapafu (nimonia) wakiwa 1,029,548 sawa na asilimia 7.4.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika shule mbalimbali za msingi na sekondari, ulibaini asilimia kubwa ya wanafunzi hujinunulia vitafunwa na vinywaji mbalimbali kipindi cha mapumziko ya saa nne asubuhi na mchana.
Baadhi ya vyakula hivyo ni pamoja na juisi, biskuti, ubuyu, barafu, mihogo, vitumbua, sambusa za viazi, kachori pamoja na vitu vingine vidogo vidogo ambavyo hata hivyo havina umuhimu kwa afya zao.
Uchunguzi ulibaini baadhi ya juisi zina ukakasi, kemikali nyingi ambazo zimekuwa zikiuzwa madukani kiholela, zikiingizwa nchini kwa wingi na nyingine kutengenezwa katika viwanda bubu vya ndani.
Baadhi ya wauzaji wa bidhaa hizo waliliambia Mwananchi kuwa wamekuwa wakiuza boksi nyingi kwa siku.
“Kwa siku nanunua boksi za juisi hizi moja Sh3,500 ndani zinakaa 24 na ninauza Sh300 kila mojawapo. Na hizi nyingine (za chupa fupi) nanunua Sh5,500 nauza Sh500 kila moja nazo zinakaa 24,” anasema Anual Raphael mfanyabiashara katika moja ya shule za msingi jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya juisi zilizokutwa zikiuzwa sokoni, nembo zake za ubora zinaonyesha ni feki’ na hazitambuliwi na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Baadhi ya wakazi wanaozunguka maeneo hayo, wamesema watoto wamekuwa wakinywa juisi hizo kwa wingi, suala ambalo mzazi kama angeona asingekubaliana nalo.
“Unakuta mtoto anakunywa vinywaji vyenye sukari nyingi, ambayo hata mtu mzima huwezi kuvumilia kumaliza chupa moja, anakunywa na kuongeza nyingine. Hii ni hatari kwa kuwa wanajipimia wenyewe hakuna usimamizi na mfanyabiashara anauza alimradi amefanya biashara,” amesema Abdul Omary, mkazi wa Temeke.
Uchunguzi umebaini kuna mvutano mkali kati ya wafanyabiashara hao na baadhi ya viongozi wa shule, changamoto kubwa ikiwa ni masuala mbalimbali ya usalama wa vyakula hivyo na ubora wake.
“Tunapotaka kutekeleza mwongozo wa lishe shuleni wazazi wengi hawana mwitikio, lakini wanaacha kuchanga fedha shuleni wanawapa watoto mkononi ambao wanaamua kununua vitu wanavyotaka wao, ambavyo havina hata ubora wala usalama,” anasema mwalimu (jina linahifadhiwa) wa shule ya msingi iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Ofisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Peter Kaja anawataka wazazi wawe na utamaduni wa kuchangia chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao.
“Mfano wapo wananchi wanaouza vyakula shuleni visivyo na virutubisho vinavyotakiwa kwa watoto, lakini walimu wanapotaka kuwaondoa wafanya biashara hao wanakataa kuondoka,” amesema Kaja na kuongeza;
“Kukataa huko kunakuja baada ya kupewa ruhusa kutoka kwa viongozi wa Serikali, mfano madiwani ambao wanasema wajasiriamali hao waendelee kufanya biashara maeneo ya shule kwani wananchi hao ndio waliompa kura kipindi cha uchaguzi.”
Hata hivyo, baadhi ya walimu wakuu waliohojiwa na Mwananchi kuhusu bidhaa hizo kuuzwa kiholela shuleni, walisema si wazungumzaji wakimtaka mwandishi aonane na Mkurugenzi wa Halmashauri.
Hata hivyo Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Ofisi ya Rais Tamisemi, kilipotumiwa maswali kuhusu suala hilo majibu yalikuwa kama ifuatavyo;
“Suala la uhakiki wa ubora wa vyakula, uchunguzi wa usalama wake ikiwemo uchunguzi wa uwepo wa kemikali katika vyakula, kuandaa miongozo haviko katika maamuzi ya Tamisemi.”
Hata hivyo, bado maswali mengi yanaibuka kuhusu usalama wa vyakula na vinywaji hivi, huku Serikali kupitia Tamisemi ikiwa imeajiri maofisa afya katika ngazi za halmashauri mpaka kata.
Akifafanua kuhusu maofisa afya, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe anasema suala la utoaji elimu shuleni lina utaratibu wake.
“Wapo walimu wa afya shuleni, lakini pia wako maofisa afya wanayo majukumu yao ambayo yamejikita katika usafi,” anasema,
Dk Magembe anasema licha ya kwamba suala la udhibiti wa vyakula na vinywaji liko chini ya TBS, sekta ya afya inaendelea kutoa elimu ya ulaji bora na mtindo bora wa maisha.
“Katika vitu ambavyo tunatoa elimu ni pamoja na kuepuka vinywaji vilivyoongezwa sukari kama hivi, badala yake watu watumie matunda halisi na maji ya kunywa. Pia vinywaji hivi vyenye sukari nyingi hasa kwa watoto vinaongeza hatari ya kuoza meno.
“Pia matumizi makubwa ya sukari yanahusishwa na kuongezeka uzito, magonjwa ya moyo, kisukari aina ya pili na hii ina madhara makubwa sana kwa watoto, sasa hivi tunaona ongezeko la ugonjwa wa kisukari kwa watoto na si kwamba wamerithi,” anaongeza Dk Magembe.
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ashura Katunzi anasema shirika limepewa jukumu la kusimamia na kudhibiti usalama na ubora wa bidhaa za chakula ikiwemo juisi kupitia Sheria ya Viwango Sura ya 130.
Anasema TBS imeweka mifumo ambayo ni pamoja na ithibati ya ubora kwa alama maalum, usajili wa bidhaa na maeneo ya kuhifadhi chakula, ukaguzi wa bidhaa nchi zinapotoka, ukaguzi wa bidhaa baada ya kuwasili na ukaguzi wa bidhaa katika soko.
“Ukaguzi viwandani na ithibati ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi, zinazouzwa sokoni ikiwemo shuleni zinazotoka kiwandani, huhusisha tathmini na ukaguzi wa awali wa kiwanda ili kubaini kama mifumo yake huzalisha bidhaa ni bora na salama,’’ anasema na kuongeza:
“Baada ya kufuata taratibu zote, TBS huendelea kufanya kaguzi za kushtukiza viwandani na sokoni ikiwemo maeneo hayo ya shule ili kukagua na kuchukua sampuli za bidhaa zote zilizopewa nembo ya kutumia alama ya ubora ya TBS zaidi ya mara mbili kiwandani na sokoni kwa mwaka,” anasema.
Anasema bidhaa ambazo ziko chini ya kiwango wanachukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwataarifu wazalishaji na wasambazaji na kufanya marekebisho, kuziteketeza na kuzuia kuingiza sokoni pamoja na hatua zingine mbalimbali za kisheria ikiwemo kuzisitisha na kuwapiga faini wazalishaji.