Dar es Salaam. Wakati Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Ubungo (EACLC) kikitarajiwa kuzinduliwa Agosti 2 mwaka huu, Serikali imeeleza faida za kiuchumi zitakazopatikana.
Miongoni mwa faida hizo ni kodi zitakazokusanywa kila mwaka, kukuza uuzaji wa bidhaa za ndani katoka masoko ya nje, kujenga uhusiano wa kibiashara na nchi jirani na kukuza biashara kati ya mataifa hayo.
Hayo yamesemwa leo katika mkutano wa waandishi wa habari kati ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) na EACLC kuelekea uzinduzi utakaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza, Mkurugenzi Mkuu wa Tiseza, Gilead Teri amesema kuzinduliwa rasmi kwa kituo hicho kutaongeza mapato ya serikali kupitia kodi, leseni zinazotolewa na mamlaka za serikali za mitaa na ushuru utakaokuwa unatolewa.

“Ushuru kwa sababu bidhaa yoyote iliyoongezewa thamani inayouzwa na kununuliwa huwa inalipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), Hivyo biashara kubwa itakayofanyika hapa itakuwa ana malipo ya risiti za kielektroniki (EFD) na tunatarajia kukusanya VAT katika mapato hayo,” amesema.
Pia, amesema kodi nyingine itakayolipwa ni baada ya wafanyabiashara kupata faida wakati ambao Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pia itakuwa na ofisi ndani ya jengo hilo kwa ajili ya kuwasaidia na kuwawezesha kutekeleza suala hilo kwa urahisi.
Akifafanua mapato yatakayopatikana, Teri amesema Serikali inatarajia kunufaika na mapato ya moja kwa moja takribani dola milioni 10 kila mwaka (Sh25.63 bilioni) sambamba na dola 200,000 (Sh512.6 milioni) za ushuru na tozo na ushauri
“Pia tunatarajia thamani ya biashara ya mauzo ya nje kuwa dola milioni 150 kwa mwaka (Sh384.45 bilioni) ikijumuisha bidhaa zinazoletwa nchi na kupelekwa nchi za jirani, bidhaa za Watanzania zilizouzwa nje kupitia kituo hiki na bidhaa zilizoletwa nchini na kuongezewa thamani kabla ya kuuzwa tena masoko ya nje,” amesema Teri.

Pia, Mwekezaji tayari amelipa Sh2 bilioni kama kodi ya ardhi hadi mwaka wa fedha 2024/2025, chini ya makubaliano ya uwekezaji na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Amesema uwepo wa kituo hicho pia utasaidia katika uuzaji wa bidhaa za Tanzania nje ya nchi kwani wauzaji watakuwa wakisaidiwa namna ya kufikia masoko yaliyopo kwa uhakika.
Teri amesema Kituo hiki kinatarajiwa kuwa kiunganishi kikuu cha biashara Afrika Mashariki na masoko ya kimataifa, kukuza uwekezaji wa mipakani, hasa kati ya China na nchi za Afrika Mashariki.
“Kituo hiki kitakuwa si tu cha biashara cha Dar es Salaam bali cha jumuiya ya Afrika Mashariki, tunategemea wafanyabiashara kutoka Burundi, Rwanda, Somalia
Uganda na Kenya waje kununua bidhaa katika eneo hili sambamba na wale wanaotoka nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara (Sadc),” amesema.
Alizitaka manispaa nyingine kuiga mfano huo ili waweze kupata uwekezaji wa aina huyo ili kusisimua uchumi wa maeneo husika.
“Na kituo hiki hakiwezi kuua Kariakoo, hapa kuna maduka 2,060 Kariakoo kuna maduka zaidi ya 30,000 zaidi kitaiimarisha Kariakoo na nina amini asilimia 75 ya maduka ya hapa yamechukuliwa na watu wa Kariakoo,” amesema Teri.
Amesema hofu ya kusema Kariakoo itakufa si mara ya kwanza kushuhudiwa kwani ilipozinduliwa Mlimani City, maduka yalipofunguliwa kwa kasi Sinza, mabadiliko yalipofanyika hofu kama hiyo ilikiwapo lakini hakikabadilika kitu.

Ujenzi wa kituo hiki umegharimu Sh282.7 bilioni hadi sasa huku asilimia 98.9 ya fedha hizo imetumika kwenye ujenzi na maendeleo ya kituo ambacho kina jumla ya maduka 2,060.
Mkuu wa idara ya mipango, uratibu na uchumi, kutoka Manispaa ya Ubungo, Andambike Kyomo amesema wakazi wa wilaya hiyo ni wanufaika wa moja kwa moja kwani mapato yatakayopatikana yatakwenda kutoa huduma kwa wananchi.
“Miongoni mwa huduma hizo ni kujenga barabara, vituo vya afya na kuongeza chachu ya maendeleo. Mradi huu ni wa miaka 32 kwa gharama walizowekeza baada ya muda huo eneo linarudi chini yetu,” amesema Kyomo.
Mkurugenzi Mkuu EACLC, Cathy Wang amesema kituo hicho ni kitovu muhimu kilichoanzishwa ili kuimarisha na kukuza ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.
“TISEZA na Manispaa ya Ubungo zimesaidia kutoa mwongozo wa kisera na wawekezaji motisha ambazo zimehakikisha mpango huu unawiana kikamilifu na dira ya Tanzania ya ustawi wa kiuchumi na maendeleo ya teknolojia.
Amesema kituo hico cha kibiashara chenye ukubwa wa mita za mraba 75,000 ni zaidi ya daraja muhimu la biashara linalounganisha Afrika Mashariki na masoko ya kimataifa.
Amesema kitaimarisha muunganisho wa miundombinu, kurahisisha biashara, kutaletwa bidhaa za ubora wa juu katika masoko ya Afrika na kusaidia bidhaa za Kiafrika kufikia ulimwenguni pote.
“Muhimu zaidi, Kituo kiko katika nafasi ya kimkakati ya kuinua Dar es Salaam kama lango kuu la Afrika Mashariki pia kuwa kitovu cha uchumi na biashara kwenye ukanda huu,
“EACLC tayari imetengeneza nafasi za kazi 5,000 wakati wa ujenzi na inakadiriwa kutoa ajira 15,000 za moja kwa moja kikianza na kuongeza ajira 50,000 zisizo za moja kwa moja,” amebainisha.
Amesema lengo lao ni kuwawezesha vijana wa Kitanzania kitaalamu kwa uchumi wa kisasa, kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika mapinduzi ya kidijitali na usafirishaji kwa kukuza ajira endelevu, uvumbuzi, na ujasiriamali.