INAELEZWA Yanga Princess imeshawapa taarifa wachezaji 10 ambao hawataendelea nao msimu ujao, akiwamo kinara wa ufungaji, Neema Paul.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Yanga Princess, Kibwana Matokeo, kuelekea msimu ujao wanafanya marekebisho kwenye baadhi tu ya maeneo.
Nyota hao ni Neema Paul aliyemaliza kinara wa mabao akiweka mabao 12, Danai Bhobho ambaye alitumikia Yanga kwa msimu mmoja akitokea Simba Queens, Rebeca Ajimida kutoka Nigeria ambaye hakupata nafasi ya kucheza kikosini hapo, na Lucy Pajero.
Wengine ni beki Asha Omary ambaye tayari amejiunga na Simba Queens, kiungo Veronica Mapunda, makipa Adrophina Samson na Belina Nyamwihula ambao hawakuwa wanapata nafasi ya kikosi cha kwanza.
Mshambuliaji Ariet Udong aliyecheza nusu baada ya kupata majeraha kwenye goti na alifunga mabao matatu, mwingine ni beki Diana Antwi aliyedumu kikosini hapo misimu mitatu mfululizo.
“Kuna maeneo tutafanya marekebisho ili kukiweka sawa kikosi chetu kuelekea msimu ujao, msimu uliopita ulikuwa bora kwetu, kwenye sajili tutaongeza tu baadhi yao ili kuhakikisha tunakwenda kufanya vizuri,” alisema Edna Lema.