Yanga yampigia  hesabu Mtunisia | Mwanaspoti

YANGA leo jioni imetangaz akumuongezea mkataba wa miaka miwili, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Pacome Zouzoua, ikiwa ni sehemu ya kuboresha kikosi cha msimu ujao, lakini ikielezwa kwamba sio kwa wachezaji tu, bali hata katika benchi la ufundi nako kuna watu wanashushwa.

Ndio, Yanga iliyomtambulisha kocha mpya, Romain Folz jana jioni, baada ya awali kumtambulisha kiungo kutomka Zanzibar, Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’, imeelezwa kwa sasa ipo mbioni kushusha mtaalamu kutoka Tunisia ili kuliongezea benchi la ufundi chini ya Mfaransi mwenye umri wa miaka 35.

Habari za kuaminika kutoka Yanga zinasema kuwa, benchi la ufundi linakwenda kuongezewa nguvu, huku moja kati ya hesabu zilizopo sasa ni kumrudisha kwa aliyekuwa daktari wa viungo, Youssef Ammar.

Kocha huyo ambaye alianza kufanya kazi na Nasreddine Nabi aliyeitumikia Yanga kwa misimu miwili na nusu ya mafanikio, lakini baada ya Mtunisia huyo kaagana na kikosi yeye aliendelea kusalia na hata alipoajiriwa Miguel Gamondi msimu wa kwanza ndipo kocha huyo wa viungo alifikia makubaliano na Yanga na kuondoka.

Taarifa za ndani ya Yanga ililiambia Mwanaspoti  kuwa sababu ya kurejeshwa kwa Ammar ni ubora alionao.

“Maboresho hayataishia katika kikosi kwa maana ya wachezaji pekee, tutaboresha pia benchi la ufundi, wapo ambao watakuja na kocha mpya, lakini wapo tutawaongeza baada ya majadiliano na kocha wetu,” kilisema chanzo hicho kutoka Yanga na kuongeza;

“Nadhani mlimsikia Rais (Hersi Said) hivi karibuni aliweka wazi kwamba, tutakuwa na timu kubwa zaidi msimu ujao, mfano kuna yule daktari wa viungo kutoka Tunisia (Yousef) alikuwa hapa kisha akaondoka enzi za Gamondi, lakini bado aliendelea kufanya kazi kubwa za wachezaji wetu, tunafikiria kumrudisha aje aongeze nguvu zaidi ni kati ya watu bora tuliowahi kuwa nao .”

“Hata wachezaji wanatuambia yule jamaa alikuwa na mchango mkubwa sana kwao, bahati nzuri alishajua hadi Kiswahili hivyo aliweza kufanya kazi na yeyote.” 

Mwanaspoti linafahamu baada ya kuondoka Yanga bado iliendelea kumtumia Ammar na ndiye aliyesimamia upasuaji wa beki Yao Kouassi, aliyekuwa majeruhi na kwenda kutibiwa Tunisia.

Wakati yuko Yanga alisimamia upasuaji wa Abuutwalib Mshery alipopata jeraha la goti na Yacouba Songne wakati alipokuwa akichezea kikosi hicho na wachezaji wote walirejea katika hali zao kwa haraka.

Kilichomuondoa Ammar ndani ya Yanga ni baada ya kumalizika kwa mkataba na uongozi kipindi hicho haukuwa tayari kumuongezea.

Na iwapo atarajea kikosini, ataungana na kocha mpya Romain Folz aliyetambulishwa juzi baada ya Mwanaspoti kumfichua mapema tangu wiki mbili zilizopita sambamba na kocha wa makipa Majdi Mnasria aliyetua na kocha huyo aliyewahi kufundisha klabu kadhaa barani humu.

Klabu ya Yanga inayodaiwa imeshakamilisha usajili wa nyota watano wakiwamo wanne wa kigeni, Celestin Ecua, Mohamed Doumbia, Balla Mousa Conte na Lassane Kouma, mbali na kumuongezea mkataba kiungo Mudathir Yahya na kushusha mido kutoka Zenji, Abdulnassir Abdallah ‘Casemiro’.

Yanga inatarajiwa kuanza kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano mwishoni ma mwezi huu ikipanga kwenda Misri.