Kocha Mbelgiji akiri Yanga imepata jembe!


KIKOSI cha Yanga inaendelea kusukwa kwa mashine mpya zikitambulishwa sambamba na wale waliokuwapo katika kikosi cha msimu uliopita wakiongezewa mikataba kama alivyofanyiwa Danis Nkane, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua, lakini kuna mido mmoja aliyetua ghafla Jangwani.

Ndio, Yanga imeshakamilisha dili la kiungo Lassine Kouma ambaye wakati wowote kuanzia leo ataanza safari ya kuja nchini kufanyiwa utambulisho sasa kocha anayemnoa katika timu ya taifa, amekubali hesabu za mabingwa hao wa Tanzania kwa kumsajili kwa kusema wamelamba dume.

Kocha aliyezungumza hayo ni Mbelgiji Tom Saintfiet, ambaye miaka ya nyuma mashabiki wa Yanga walimpa jina la mtakatifu Tom, ameliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kwamba kama angekuwa na namba ya viongozi wa klabu hiyo angewapongeza kwa usajili bora.

Saintfiet ambaye kwasasa ndiye kocha wa timu ya taifa ya Mali, alisema Kouma ni kiungo fundi wa juu ambaye amezaliwa na kipaji kikubwa na kwamba huo ni usajili bora kwa Yanga ambayo aliifundisha kwa mafanikio na kwa muda mfupi.

Kocha huyo mwenye msimamo mkali, alisema Kouma anajua kutengeneza nafasi lakini kitu hatari zaidi anaweza kuibeba mechi kwa maamuzi ya miguu yake akiwa na ujuzi hata wa kufunga mabao.

Alisema Yanga imepata kiungo mzuri ambapo mashabiki wa timu hiyo ambao anawakumbuka kwa moyo wa kupenda wachezaji wao watafurahia kwa kuliimba jina lake.

“Ndio namjua Lassine, ni mchezaji wangu timu ya taifa ni kijana mdogo ambaye ana kipaji kikubwa, nimesikia kwamba anakwenda Tanzania lakini anakwenda kujiunga na timu yangu ya zamani ni kitu kimenifurahisha zaidi,” alisema Saintfiet na kuongeza;.

“Ningekuwa na namba za viongozi wa Yanga ningewapongeza lakini ningewaambia wamtunze ni kiungo anayejua sana soka, anaweza kutengeneza nafasi lakini anaweza kufunga pia.

“Kuna mechi ambazo timu unaona iko chini lakini ukiwa na Lassine (Kouma), ana uwezo wa kuirudisha timu mchezoni, mbunifu sana akiwa kwenye nusu ya wapinzani, nakumbuka vaibu la mashabiki wa Yanga, wanapenda sana timu yao, nadhani wataimba sana jina lake.

Aidha, Saintfiet alimtaka kiungo huyo wa zamani wa Stade Mallien kujipanga na ushindani zaidi kwenye ligi ya Tanzania, akisema atatakiwa kuchangamka kwa haraka.

“Ligi ya Tanzania ni ngumu sana, watu wanashindana sana , nakumbuka timu inapokutana na Yanga inakuwa kama imeambiwa ukipoteza mechi hii unashuka daraja, haitakuwa rahisi kwake atatakiwa kupambana sana.”

Msimu uliopita, Kouma akiwa na Mallien alifanikiwa kuhusika kwenye mabao 16 akifunga saba na kutoa asisti tisa.