Kwa nini uwekezaji kwenye rasilimaliwatu

Dar es Salaam. Jitihada za Tanzania kujenga uchumi imara na wa kisasa, zinaweza zisifue dafu endapo haitaifanyia kazi changamoto ya rasilimaliwatu, nguvu kazi yenye ujuzi, maarifa na uwezo wa kutekeleza majukumu kwa tija ili kufikia ndoto ya kuwa Taifa la kipato cha kati cha juu kufikia 2050.

Licha ya Taifa kupiga hatua katika ujenzi wa miundombinu na kuvutia uwekezaji, maendeleo hayawezi kufikia viwango vinavyotakiwa iwapo pengo la rasilimaliwatu halitashughulikiwa kikamilifu.

Kwa mujibu wa ripoti za kitaifa na kimataifa, Tanzania ina idadi kubwa ya watu, hususani vijana, lakini wengi hawana ujuzi wa kutosha kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wako chini ya umri wa miaka 35, lakini asilimia kubwa ya kundi hilo halina ajira rasmi wala ujuzi wa kujiendesha kiuchumi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi hali hiyo inaashiria pengo kubwa kati ya idadi ya watu na ubora wa rasilimaliwatu waliopo, hivyo wamependekeza kufanyika uwekezaji makini, wa kimkakati na wa pamoja kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla ili pengo hilo lizibwe.

Mtaalamu wa uchumi, Kimiro John amesema kuwekeza katika rasilimaliwatu yenye tija si hiari ni sharti la msingi kwa Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo.

Amesema sekta kama za viwanda, Tehama, afya, ujenzi na nishati zinakabiliwa na uhaba wa wataalamu waliobobea, huku wajasiriamali wengi wakikosa maarifa ya msingi ya biashara na uongozi wa kidijitali.

John amesema Taifa litakalowekeza katika elimu, ujuzi na ubunifu wa watu wake ndilo litakalosimama imara kiuchumi, kisiasa na kijamii katika zama hizi za mabadiliko ya kasi.

“Rasilimaliwatu ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Taifa lenye watu wenye tija lina uwezo mkubwa wa kuzalisha, kuvumbua na kusimamia maendeleo endelevu ndiyo maana tunahitaji kuwekeza kwenye elimu,” amesema.

“Uwekezaji katika elimu bora na mafunzo ya ujuzi unawawezesha vijana kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali. Hii husaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana, ambayo ni moja ya matatizo makubwa kwa Tanzania,” amesema.

Hoja kama hiyo ilitolewa hivi karibuni na mfanyabiashara Rostam Aziz wakati wa uzinduzi wa Dira ya Taifa 2050. Alisema ili Tanzania ipige hatua za haraka katika karne ya 21, hakuna budi kuwekeza katika rasilimaliwatu, hususani vijana.

Alipendekeza kuanzishwa Mfuko wa Maendeleo ya Vipaji, wenye bajeti ya takribani Dola milioni 70 za Marekani kila mwaka, kwa kipindi cha miaka kadhaa.

Rostam alisema kupitia mpango huo vijana 1,000 wenye uwezo mkubwa katika nyanja za kimkakati kama vile uhandisi, akili mnemba (AI), sayansi ya takwimu, fedha na kozi nyinginezo zitakazokidhi mahitaji ya kukuza rasilimaliwatu katika harakati za kuleta maendeleo ya nchi watatambuliwa na kujengewa misingi ya kuimarika zaidi.

Kwa upande wake, Dk Konga Gilman amesema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2050 na ajenda ya Maendeleo Endelevu (SDG) haviwezi kutekelezwa bila watu wenye uelewa, weledi na uadilifu, hivyo rasilimaliwatu yenye tija ndiyo injini ya kufanikisha sera, mikakati na mipango ya maendeleo.

Amesema dunia inabadilika kwa kasi kupitia mapinduzi ya kidijitali na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na Tanzania haitoweza kushindana kiuchumi, kiteknolojia na kisera bila kuwa na watu waliobobea katika nyanja muhimu.

Kukabiliana na hilo amesema Tanzania inahitaji watu waliobobea kwenye sayansi, teknolojia na sera za mazingira ili kuleta maendeleo.

“Uchumi wa sasa unategemea maarifa na uvumbuzi. Sekta nyingi zinazochochea uchumi kama nishati jadidifu, Tehama, viwanda vya kisasa na huduma za kifedha zinahitaji watu waliobobea katika taaluma hizo. Bila kuwaandaa vijana katika maeneo hayo, Taifa haliwezi kuwa na uchumi unaoshindana kimataifa,” amesema.

Amesema: “Kwa sasa miradi mingi mikubwa ya kitaifa hutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi, tukijenga kizazi cha wataalamu wa ndani wenye uwezo wa kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa bila kuagiza maarifa kutoka nje. Hii itaokoa fedha nyingi za kigeni na kuongeza ajira kwa Watanzania.”

Julai 26, 2023 akifungua mkutano wa kimataifa wa rasilimaliwatu, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Bara la Afrika haliwezi kujikomboa kiuchumi kama halitawekeza kwenye rasilimaliwatu, hivyo aliyahimiza mataifa ya Afrika kuwekeza kwa watoto tangu wanapozaliwa hadi wanapokwenda shule.

Alisema ili kuhakikisha wanaweka msingi mzuri, wanapaswa kuwa na maandalizi mazuri ya elimu hasa ya awali kwa ajili ya kuwaandaa watoto kimwili, kiakili, kijinsia na kiubunifu.

Samia alisema kwa sasa, Afrika ndiyo bara lenye vijana wengi zaidi na takwimu zinaonyesha ifikapo mwaka 2050, Afrika itatoa nchi 10 zenye idadi kubwa ya vijana duniani.