Dar es Salaam. Msaada rasmi wa maendeleo kwa ajili ya afya (ODA) unaotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unaweza kushuka na kufikia kiwango cha chini zaidi kwa muongo mmoja.
Msaada wa afya unakadiriwa kupungua kwa hadi asilimia 40 mwaka 2025 ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2023, kutoka zaidi ya Dola bilioni 25 (sawa na Sh63.9 trilioni) hadi takriban Dola bilioni 15 (Sh38.3 trilioni) kulingana na makadirio ya WHO.
Hii ni chini hata ya msaada wa afya wa ODA wa mwaka 2015, ambao ulikuwa zaidi ya Dola bilioni 18 (Sh46 trilioni).
Makadirio hayo yamewasilishwa mapema mwezi huu, wakati wa kongamano la INSPIRE lililoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Asia.
Hali hii itaathiri pakubwa nchi nyingi zenye kipato cha chini, ambazo hutegemea kwa kiasi kikubwa misaada ya nje katika sekta ya afya na inahatarisha kuongeza uwezekano wa watu kutumia fedha zao binafsi kwa ajili ya huduma za afya.
Hata hivyo, kuna njia ambazo nchi zinaweza kutumia kuongeza matumizi ya ndani kwenye afya.
Kupungua huku kunatokana na kupunguzwa kwa kiwango kikubwa kwa ufadhili kutoka kwa baadhi ya nchi kubwa wahisani duniani, ikiwemo Marekani ambayo ni mfadhili mkuu wa afya kwa kiwango cha kitaifa pamoja na baadhi ya nchi za Ulaya.
Hata hivyo alipoulizwa kuhusu hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Tanzania, Dk Seif Shekalaghe amesema kupungua kwa misaada hiyo hakuna kitu kitakachokwenda tofauti, “Serikali ina wajibu wa kuhudumia wananchi na hakuna huduma ambayo itatetereka.”
Hali hii itaziathiri sana nchi zenye kipato cha chini ambazo hutegemea misaada ya nje kwa ajili ya sekta ya afya na itaathiri uwezo wao wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa, huku pia ikiongeza hatari ya watu kulazimika kutumia fedha zao binafsi kwa ajili ya mahitaji yao ya kiafya.
Matumizi ya fedha binafsi kwa ajili ya huduma za afya, yanaweza kuwasukuma watu binafsi au familia kwenye umasikini, hasa pale gharama za matibabu zinapokuwa kubwa.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa ongezeko la matumizi ya afya katika nchi zenye kipato cha chini kati ya mwaka 2000 na 2022, liliendeshwa na msaada wa nje pamoja na matumizi binafsi, ambayo yalichangia zaidi ya asilimia 40 ya matumizi yote ya afya katika nchi za kipato cha chini na cha kati.
Katika eneo la Afrika, matumizi binafsi ya fedha yalichangia zaidi ya asilimia 50 ya matumizi yote ya afya katika nchi 11, zikiwemo Guinea ya Ikweta, ambayo imeainishwa kama nchi ya kipato cha juu cha kati na Benki ya Dunia.
“Maana yake ni kwamba, nchi zinapaswa kutumia zaidi kwenye afya. Basi zinapaswa kuipa kipaumbele bajeti ya umma ya afya,” amesema Mkurugenzi wa utawala, ufadhili, uchumi, huduma za afya msingi na huduma za afya kwa wote – WHO, Kalipso Chalkidou wakati wa mkutano wa kongamano la INSPIRE.
Chalkidou anashauri kuwa baada ya kupunguzwa kwa misaada, viongozi kadhaa wa afya wameongeza wito wa kutumia mbinu za ufadhili mchanganyiko, pamoja na kodi za afya ili kuongeza bajeti ya afya kutoka vyanzo vya ndani.
Hata hivyo, kuna vyanzo vingine vya ufadhili. Kwa upande wa kodi, kwa mfano nchi zinaweza kuboresha ukusanyaji wa kodi, ikiwa ni pamoja na kushughulikia upotevu wa fedha kupitia njia zisizo halali.
Nchi pia zinaweza kuongeza matumizi yao ya afya, iwapo zitaondokana na mzigo mkubwa wa riba za madeni kupitia msamaha wa madeni au mabadiliko katika masharti ya ulipaji.
Suluhisho jingine ni matumizi ya Special Drawing Rights (SDRs), ambazo ni akiba za kimataifa zinazoshikiliwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambazo nchi zinaweza kutumia kukabiliana na majanga au kuzipeleka kwenye benki za maendeleo za kimataifa ili kuongeza uwezo wa benki hizo kukopesha nchi.
Nchi pia zinaweza kuongeza matumizi ya mikataba ya “debt-for-development swaps,” ambapo nchi hupunguziwa deni na badala yake hutumia fedha hizo kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo kama afya.
Mekanismi hizi tayari zinatumika kusaidia nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi au kuimarisha sekta ya elimu. Lakini zinaweza pia kuwekwa ili kuisaidia sekta ya afya, alisema Chalkidou.
Changamoto kubwa ni kupanua matumizi ya suluhisho hizi. “Tuna tatizo la kiwango cha utekelezaji,” Chalkidou ameiambia Devex. “Kiwango cha suluhisho tulizo nazo, kiko chini sana ukilinganisha na ukubwa wa pengo tunaloliona.”