STAA wa zamani wa Yanga, Ladslaus Mbogo ameshindwa kuficha hisia alizonazo, akimtaja beki wa kati wa timu hiyo, Ibrahim Bacca kuwa mchezaji anayetikisa katika nafasi hiyo kwa miaka ya sasa, huku akilia na soka la Mwanza.
Mbogo aliyewahi kutamba na timu hiyo kwa mafanikio, akicheza pia soka la kulipwa nje ya nchi kwa kukipiga Olympique Star ya Burundi na kuhitimishia kazi kwa kuitumikia Toto Africans baada ya awali kupita Kagera Sugar, Rhino Rangers na timu ya Mkoa wa Mwanza.
Kwa sasa Mbogo anaendelea na shughuli za michezo akisimamia kituo chake cha vijana, Mbogo Sports Academy na akizungumza na Mwanaspoti, alisema kwa miaka ya sasa, Bacca ndiye beki bora kwa muda wote kutokana na kiwango anachoonesha kwa timu yake na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Alisema pamoja na kazi iliyowahi kufanywa na mabeki wengine waliowahi kupita Yanga akiwamo yeye, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na John Mwansasu, Bacca anairejesha Yanga katika zama za wakongwe hao.
“Ni beki ambaye kwa sasa yuko katika kiwango bora, naweza kusema ndiye beki anayeirudisha Yanga enzi za wakongwe kina Cannavaro, anatumia akili, nguvu na maarifa awapo uwanjani,” alisema Mbogo.
Mkongwe huyo aliongeza, ligi ya sasa imebadilika kwa kuwa wananchi wametambua umuhimu wa mpira na kuongeza uwekezaji hali ambayo inamfanya mchezaji kujituma.
Alisema pamoja na maendeleo hayo, lakini anasikitika kuona mkoa wake wa Mwanza ukirudi nyuma kwenye soka, kwakuwa badala ya kuongezeka timu, zinapungua.
“Hali hii inaleta sintofahamu, Mwanza ilikuwa kitovu cha michezo, lakini kwa sasa tunapiga hatua 100 nyuma, hii ni kwa sababu uongozi kutegemea mpira badala ya kutegemewa na mpira,” alisema Mbogo na kuongeza;
“Masilahi binafsi, lakini kutothamini mchango wa wenye taaluma ya mpira badala yake wanasikilizwa wenye kipato hata kama hajui masuala ya soka, lazima tubadilike turudishe heshima,” amesema nyota huyo.