Mpanzu arejea Simba kibosi, mchongo mzima upo hivi

NYOTA w Simba wameanza kurejea kutoka mapumzikoni ili kuanza maandalizi ya msimu mpya wa mashindano wa 2025-2026, huku kiungo mshambuliaji, Ellie Mpanzu akishtua zaidi kwa kurudi kibosi.

Nyota huyo raia wa DR Congo aliyejiunga na Simba kupitia dirisha dogo la msimu uliopita na kuhusika katika mabao 10, akifunga manne na kuasisti sita alikuwa akitajwa huenda asingerejea, huku Yanga ikitajwa, lakini kile kilichofanywa na mabosi wa klabu hiyo imemaliza utata kabla hajatua leo Ijumaa.

Kiungo mshambuliaji huyo amemaliza ule utata uliokuwepo karibu wiki  nzima juu ya tetesi kwa kwamba uhenda asingerejea tena Msimbazi kutokana na ishu ya mkataba aliokuwanao na klabu hiyo na ile inayommiliki, huku akihusishwa na mabingwa wa Tanzania, Yanga.

Mpanzu alitua Msimbazi kupitia dirisha dogo na kuifungia mabao manne na asisti sita, huku akiwa sehemu ya kikosi kilichoandika historia ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco na ilivumishwa huenda akahamia mtaa wa pili.

Hata hivyo ni kwamba, hakuna uwezekano wowote wa klabu yoyote ya Ligi Kuu Bara kumnasa  Mpanzu kwa ajili ya msimu ujao, Mwanaspoti limeambiwa bado ataendelea kusalia Msimbazi, huku gari na pesa zikitajwa sambamba na kuwekewa ulinzi mkali tangu alipotoka mapumzikoni kwao DR Congo hadi alipotarajiwa kuwasili jana kwenye Uwanja wa Ndege, jijini Dar es Salaam.

Ipo hivi. Inaelezwa kuwa kuanzia jana Ijumaa alivyowasili Jijini Dar es Salaam kujiunga na Simba kuna mambo mazuri watamfanyia Mpanzu ambayo yatamfanya aishi kibosi nchini.

Mwanaspoti limeelezwa kuwa tayari Simba imelipa deni la Dola 70,000 sawa na Sh181milioni  iliyokuwa inadaiwa na klabu ya Demver SPRL ya DR Congo, alikotokea winga huyo ambaye siku chache zilizopita ilizushwa katika mitandao ya kijamii kwamba huenda akaibukia timu moja iliyoko Top 4 ya Ligi Kuu Bara.

Baada ya Simba kumsajili Mpanzu kwa mkataba wa miaka miwili ilitakiwa ilipe klabu ya Demver SPRL Dola 100,000 sawa na Sh.258 milioni, lakini badala yake ilitoa Dola 30,000 ambazo ni Sh77 Milioni tu, jambo ambalo lilionekana kuleta changamoto kwenye mipango ya nyotya huyo kusalia Msimbazi.

Chanzo cha ndani kimeliambia Mwanaspoti kuwa: “Mpanzu anawasili Ijumaa (jana) Julai 25, kujiunga na timu kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, Simba tayari ilishalipa deni kwa hiyo mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi, wataendelea kumuona mchezaji huyo akivaa jezi nyekundu.”

Ukiachana na pesa iliyolipwa kwa klabu hiyo pia moja ya kipengele  kilichokuwepo katika mkataba wa Mpanzu, uongozi wa Simba ulimuahidi gari la kutembelea, ahadi ambayo imedaiwa itatimizwa siku chache zijazo atembee kibosi.

“Gari lake lipo tayari atakabidhiwa, ndio maana tunasisitiza Mpanzu ataendelea kusalia Msimbazi na zile taarifa ambazo zilikuwa zinasambaa mtandaoni kwamba anaondoka kwa sasa hazitakuwa na nguvu tena,” kilisema chanzo hicho.

Huku taarifa nyingine zikidokeza kuwa tangu alipoondoka DR Congo alipokuwa katika mapumziko, aliopewa ulinzi wa maana wa mtu wa kumsindikiza kuja naye Dar es Salaam ambapo kwenye Uwanja wa Ndege angepokelewa pia na ulinzi mwingine wa kumfikisha klabuni salama.

“Huu ni utaratibu ulioanzishwa kwa siku za karibuni na Simba kwa nia ya kuwalinda wachezaji kutokana hizi hila za baadji ya timu kuwabeba wachezaji wanahusishwa na klabu yetu. Sio Mpanzu tu, kila mchezaji hata wale wapya wamwekuwa wakiwekewa ulinzi mara wanapowasili,” kilisema chanzo hicho kutoka Simba kilichoomba kuhifadhiwa jina, kilichosisitiza Mpanzu yupo sana Msimbazi.

Msimu uliyopita Mpanzu alimaliza na mabao manne na asisti sita, kiwango kiliwavutia mashabiki, hivyo tetesi zilizokuwa zinaendelea huenda akatua Yanga zilikuwa zinawapa presha ila kwa sasa taarifa njema kwao ni Simba kumalizana na klabu aliyokuwa ametokea.

Ukiachana na Mpanzu kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Joshua Mutale naye anatarajiwa kurejea nchini wikiendi hii akitokea kwao Zambia, mchezaji huyo ligi iliyopita alimaliza na asisti mbili ambapo kiwango chake alianza kukionyesha mechi za mwishoni.