NYAKATI za sayansi na teknolojia kama mtu anataka kipaji chake kiende mbali anahitaji ubunifu na kujua mashabiki wake wanahitaji kitu gani. Ndivyo ilivyo kwa baadhi ya wanasoka wanaoweza wakapata mamilioni nje ya kazi hiyo.
Kupitia mitandao ya kijamii kama Instagram, TikTok, Facebook na mingineyo inaweza ikawatoa kwa kuziposti kazi zao ilimradi zipendwe na kupokewa na mashabiki basi mambo yao yanakuwa bambam.
Mfano mzuri ni msanii mrembo kutoka Afrika Kusini anayejulikana kwa jina la Tyla aliyekuwa anaposti nyimbo zake katika mtandao wa TikoTok kisha akapata umaarufu na amefanikiwa kunyakua tuzo za Favorite Afrobeats Artist katika tuzo za American Music 2025.
Ukija Kibongobongo kuna staa anayeitwa Kili aliyeanza kuimba nyimbo za Kihindi katika mitandao kijamii zikampa umaarufu hadi akawa anaalikwa kwenda katika matamasha nchini India na baadaye akaonekana katika tamthilia ya Jua Kali.
Mwingine maarufu kama Zerobrainer0 – Mtanzania wa kwanza kupostiwa na staa mkubwa duniani, Cristiano Ronaldo, anayekipiga Al-Nassr. Zerobrainer0 anaigiza kwa kuchezea mpira na kupiga chenga na akifunga anashangilia kwa staili ya Ronaldo. Kupitia hilo alichaguliwa kuiwakilisha Afrika kama sehemu ya burudani katika mashindano ya dunia na aliwahi kupata tuzo ya mbunifu wa video nzuri katika mtandao wa TikTok.
Mwanaspoti linakuletea baadhi ya wanasoka ambao wana vipaji vikubwa na ushawishi kwa mashabiki na endapo wakiamua kuwekeza nguvu wanaweza wakapiga pesa ndefu nje ya soka wanalolitumikia.
Kiungo wa Yanga, Denis Nkane na beki wa klabu hiyo, Kibwana Shomari wanatamba katika mitandao ya kijamii kuhusiana na pambano lao la vitasa lililotarajiwa kupigwa jana, Julai 26, 2025 jijini Dar es Salaam.
Kabla ya pambano hilo wawili hao wametengeneza video nyingi za vichekesho wanazozirusha katika mitandao ya kijamii hadi wakapata tangazo la maji katika kampuni moja lililowaingizia pesa.

Nkane aliwahi kuzungumzia hilo akisema: “Niliwahi kuigiza katika kikundi fulani hivi na video zipo Youtube, ila wengi hawajui na siwezi kukuambia. Napenda kufanya vichekesho, ila kwa sasa nguvu kubwa naiweka katika mpira wa miguu.”
Winga aliyemaliza mkataba wake Namungo ni fundi wa kuimba. Akiwa kambini na timu basi wachezaji wanaomzunguka wanapata burudani ya kutosha na endapo akiamua kuwekeza nguvu katika hilo linaweza kuwa sehemu yake nyingine ya kujipatia kipato.
Abushee anasema: “Napenda kuimba, ni vile nakosa muda wa kuwekeza nguvu katika suala hilo. Muda mwingi nakuwa nafanya mazoezi kwa ajili ya mpira wa miguu na mechi, ila wanaonizunguka ukiwauliza watakwambia ninavyoimba wanaonaje, ingawa naiona fursa kupitia mitandao ya kijamii.”
Mchezaji wa KMC, Deusdedit Okoyo ni fundi wa kupiga gitaa, jambo linalowafurahisha wachezaji wenzake katika kikosi hicho cha Manispaa ya Kinondoni.
Okoyo anasema: “Gitaa wakati mwingine linanipa utulivu. Huwa napenda kupiga muda ninaopumzika.”
Kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Haruna Niyonzima licha ya ufundi alionao katika mpira wa miguu ni mtaalamu wa kuigiza kwani aliwahi kucheza filamu ambayo ilitikisa iliyokuwa inajulikana kama The Ring aliyoigiza na mzazi mwenzake msanii maarufu hapa nchini anayejulikana kwa jina la Marry Bliz.

Mwanaspoti liliwahi kumfanyia mahojiano na Niyonzima na akasema: “Filamu hiyo imebeba uhalisia wa wanaume wengi. Kama watu watapata muda wa kuifuatilia kwa umakini itawafunza, lakini pia ninaimba muziki, naingia studio narekodi na nimewahi kufanya kolabo na mwanamuziki wa Rwanda anaitwa Jay Pole wa Hip Hop.”
Winga wa Simba, Joshua Mutale katika mitandao ya kijamii zimekuwa zikionekana video za vichekesho fupifupi anazopenda kuzifanya ikiwemo kudansi na aliwahi kuulizwa kama anafikiria kufanya vichekesho na jibu lake lilikuwa hivi.
“Napenda tu kuchekesha na kuhakikisha kila mtu anayekuwa karibu yangu anapata furaha, ila sifikirii kufanya kazi hiyo. Kwa sasa napambana kucheza mpira wa miguu kwa kiwango kikubwa.”
MOHAMED HUSSEIN ‘TSHABALALA’
Aliyekuwa nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ anayetajwa kusaini mkataba wa miaka miwili Yanga aliwahi kukiri anapenda kazi ya UDJ: “Isingekuwa mpira wa miguu ningekuwa DJ ndiyo kazi niliyokuwa naipenda.”

Kiungo wa kati wa Kagera Sugar, Abdallah Mfuko anapiga gitaa na kuimba nyimbo mbalimbali za wasanii na zipo anazowaimba wachezaji wenzake na ni kama burudani zingine zimekuwa zikirushwa katika mitandao ya kijamii. Endapo akiamua kulikomalia hilo anaweza akawa anaingiza mkwanja.
Hao ni baadhi tu ya mastaa, lakini kuna wachezaji wengi ambao wanafanya vitu tofauti na vinapendwa na jamii kama beki wa Yanga, Dickson Job (mitindo), kiungo aliyemaliza mkataba na JKT Tanzania Maka Edward (mitindo).