Wanafunzi watano wafariki kwa kugongwa na basi, tisa wakijeruhiwa

Mbeya. Wanafunzi watano wa shule ya sekondari Chalangwa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kugongwa na basi la kampuni ya Safina Coach, wakati wakifanya mazoezi ya asubuhi ‘Jogging’.

Ajali hiyo imetokea leo Julai 26 majira ya saa 11 alfajiri katika barabara kuu ya Chunya – Mbeya, ambapo basi hilo lililokuwa likitokea Chunya kwenda jijini Mbeya na liliwagonga wanafunzi hao waliokuwa wakifanya mazoezi ya mchakamchaka.

Akithibitisha ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbert Siwa amesema wanafunzi watano walifariki papo hapo.

Amesema katika ajali hiyo, tisa walijeruhiwa na saba bado wanaendelea na matibabu katika kituo cha Afya cha Chalangwa na kwamba baada ya tukio hilo, dereva wa basi hilo amekimbia na anasakwa na Jeshi la Polisi.

“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa basi, Abdul Hassan kushindwa kulimudu gari hivyo kusababisha kwenda kuwagonga wanafunzi waliokuwa wanafanya mazoezi ya kukimbia (Jogging) Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta dereva ambaye amekimbia mara baada ya kusababisha ajali hiyo,” amesema Kamanda huyo.

Waliofariki katika ajali hiyo ni Seleman Ernest, Samwel Zambi, Kelvin Mwasamba, Hosea Mbwilo na Amina Ulaya, huku majeruhi wakiwa ni Benard Mashaka, Lilian Raymond, Kenedy Masoud, Vicent Baraka, Siwema Nasibi, Alex Peter, Dethani Adam, Getruda Mwakyoma na Farida Mwasongole.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga amepiga marufuku shule au vikundi vyovyote vya michezo kukimbia barabarani badala yake watumie viwanja vilivyotengwa.

Ameongeza kuwa Serikali itagharamia shughuli za mazishi na kusimamia gharama za matibabu kwa majeruhi hao.

Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Chalangwa, Dk Ernest Fraiton amesema wamepokea miili mitano, ikiwa ni msichana mmoja na wavulana wanne na majeruhi tisa.

Mkuu wa Shule hiyo, Solomon Eliah amesema wamekuwa na utaratibu wa kila Jumamosi wanafunzi kukimbia ikiwa ni njia ya kuwajenga kiafya katika utimamu wa mwili.

“Katika mazoezi ya leo walikuwapo walimu wawili wakiwaongoza, huu ulikuwa utaratibu katika kuwaweka sawa kiafya,” amesema Mkuu huyo.

Mmoja wa wananchi Victor Nsemwa, ameiomba Serikali kuweka alama za barabarani haswa maeneo yaliyopo karibu na shule ili kuepusha ajali zisizo za lazima.