WAZIRI KOMBO AFUNGUA MILANGO MIPYA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA RWANDA KUPITIA MKUTANO WA JPC KIGALI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amefungua rasmi Mkutano wa 16 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Rwanda, uliofanyika tarehe 26 Julai 2025 jijini Kigali, Rwanda.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Waziri Kombo ametoa salamu za kindugu kutoka kwa Serikali na Wananchi wa Tanzania kwa Serikali ya Jamhuri ya Rwanda, huku akitoa shukrani za dhati kwa mapokezi ya ukarimu na mazingira mazuri ya mkutano huo.

Waziri Kombo amebainisha kuwa miradi ya pamoja ya kimkakati inayotekelezwa na nchi hizo mbili, ikiwemo Mradi wa Umeme wa Rusumo, kituo cha pamoja cha forodha cha Rusumo (OSBP), pamoja na reli ya kisasa (Standard Gauge Railway – SGR), kuwa ni vielelezo vya mafanikio ya ushirikiano wa muda mrefu.

Licha ya mafanikio hayo, Mhe. Kombo amesisitiza kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuendeleza ushirikiano huo, hasa katika maeneo ya biashara, uwekezaji, kilimo, afya, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), nishati, utalii na miundombinu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda, Mhe. Balozi Olivier Nduhungirehe, ameeleza kuwa uhusiano kati ya Rwanda na Tanzania una historia ya kina inayojengwa juu ya maadili ya pamoja, undugu wa karibu, na maono ya maendeleo ya pamoja.

Waziri Nduhungirehe pia amesisitiza mchango mkubwa wa Tanzania kama mshirika wa kimkakati wa biashara na maendeleo ya Rwanda, akieleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mizigo ya Rwanda husafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Aidha, amepongeza hatua ya kufunguliwa kwa Ofisi ya Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) mjini Kigali.