Azam FC yaanza msako mpya

KIKOSI cha Azam kinaingia rasmi kambini leo ili kuanza maandalizi ya msimu ujao (Pre Season), huku kikibeba matumaini kwa matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam, baada ya ujio wa benchi jipya la ufundi chini ya Mkongomani Florent Ibenge.

Azam inaanza maandalizi hayo ikiwa chini ya Ibenge aliyetambulishwa ndani ya kikosi hicho Julai 5, 2025, akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan na kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine zaidi.

Ibenge amejiunga na timu hiyo akichukua nafasi ya kocha wa zamani wa RS Berkane, FAR Rabat, Raja Casablanca, ES Setif, Olympique Club de Khouribga na Wydad Casablanca, Rachid Taoussi raia wa Morocco, aliyejiunga nayo Septemba 7, 2024.

Kocha huyo mzoefu, tayari amekamilisha benchi lake la kufanya naye kazi, ambapo kocha msaidizi ni Addis Worku aliyekuwa naye Al Hilal, sawa na kocha wa makipa, Rody Mountaro, huku mchambuzi mpya wa video (Video Analyst) ni Omar Boukathem.

Baada ya kusuka upya benchi hilo la ufundi, Azam inaingia kambini leo, ambapo Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kikosi hicho kina mpango wa kuweka kambi ya wiki moja ya mazoezi kwenye Uwanja wa Black Rhino uliopo, Karatu jijini Arusha.

Mtoa taarifa huyo aliliambia Mwanaspoti baada ya kambi hiyo ya muda mfupi jijini Arusha, mpango uliopo ni kwenda Morocco au Misri ikiwa ni pendekezo la benchi la ufundi, ingawa bado taratibu hizo zinaendelea kushughulikiwa kwa uharaka zaidi.

“Kipaumbele cha kwanza ni kwenda Morocco kama tulivyofanya msimu uliopita japo ilikuwa kambi ya muda mfupi, ni sehemu nzuri na tulivu, pia kuna mapendekezo ya Misri ingawa bado uamuzi wa mwisho kwa uongozi bado,” kilisema chanzo hicho.

Ikiwa timu hiyo itaenda Morocco, itakuwa mara ya pili mfululizo kwani kikosi hicho kwani msimu uliopita wa 2024-2025, kilienda pia na kukaa wiki mbili ili kujiandaa na michuano mbalimbali ya ndani na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyoshiriki.