Beki Mtanzania ataka rekodi Misri

BEKI wa Kitanzania anayekipiga Ghazl El Mahalla ya Misri, Raheem Shomari amesema anatamani kuandika rekodi akiwa na timu hiyo aliyojiunga nayo hivi karibuni akitokea KMC ya Tanzania.

Msimu wa 2023/24 Raheem aliibuka na tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi kwenye usiku wa tuzo za Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Akizungumza na Mwanaspoti, Raheem alisema kitendo cha Himid Mao kufanya vizuri kwenye ligi hiyo kimefanya wachezaji wa Kitanzania kuaminiwa, hivyo atapambana ili kuhakikisha anatekeleza imani hiyo.

Aliongeza, licha ya kuwa ni mara yake ya kwanza kucheza nje ya mipaka ya Tanzania, atapambania kupata nafasi ya kucheza.

“Mpira nchini kwetu umekua. Sasa hivi ukienda sehemu ukitokea Tanzania wanajua utakuwa miongoni mwa wachezaji wazuri, wenye nidhamu na kipaji. Kaka yangu Himid amefanya kazi kubwa sana kwenye ligi ya huku pamoja na hapa kwenye timu, kwa hiyo imekuwa inasaidia kwa kiasi chake watu kuamini kuhusu wachezaji kutoka Tanzania na vipaji vyao,” alisema na kuongeza:

“Matarajio yangu ni kupambana kupata nafasi kwenye timu na kucheza, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuja kucheza nje. Hata kwenye ligi ya nyumbani nimecheza kwa misimu miwili tu, lakini naamini nipo najifunza huku na nitapambana kupata nafasi ya kucheza.”

“Mahalla ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri na mimi hadi kuwa hapa kuna kazi nzuri pia nimeifanya, kwa hiyo nitapambana na kufuata maelekezo ya mwalimu kwenye nafasi yangu na nitashinda nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.”