Changamoto hizi kwa afya ya watoto wachanga zisipuuzwe

Licha ya mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta ya afya ya uzazi na watoto nchini Tanzania, bado kuna changamoto kubwa zinazoendelea kutishia uhai wa watoto wachanga.

Hii ni pamoja na ukosefu wa huduma bora wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na mara tu baada ya mtoto kuzaliwa. Takwimu kutoka Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto (PAT) zinaeleza kuwa asilimia 95 ya vifo vya watoto wachanga husababishwa na kukosa hewa ya oksijeni ama wakiwa tumboni au wakati wa kujifungua, jambo linaloweka bayana ukubwa wa tatizo.

Kila mwaka, Tanzania inasajili zaidi ya watoto milioni 2.3 wanaozaliwa hai, lakini takribani watoto wachanga 51,000 hufariki dunia na wengine 43,000 huzaliwa wakiwa wafu. Takwimu hizi ni za kusikitisha, hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 87 ya vifo hivyo hutokea ndani ya wiki ya kwanza ya maisha.

Ingawa Serikali imetekeleza mikakati kadhaa, kama inavyoelezwa mara kwa mara kwamba vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai, bado kiwango hicho kinahitaji kupunguzwa zaidi kwa juhudi za pamoja.

Rais wa PAT, Dk Theopista Masenge, ameonya kuwa bila kuwekeza kwenye vitengo vya huduma kwa watoto wachanga vyenye vifaa vya kisasa na wataalamu wa kutosha, taifa litaendelea kupoteza maelfu ya watoto kila mwaka. Inasikitisha kujua kuwa kuna madaktari bingwa wa watoto wasiozidi 350 kwa nchi nzima. Hii ina maana kuwa daktari mmoja anahudumia wastani wa watoto 100,000.

Hii ni hali inayoweza kuhatarisha ubora wa huduma na kuzidisha mzigo kwa watoa huduma.

Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa tatizo hili si la Tanzania pekee. Ripoti ya WHO na UNICEF ya mwaka 2023 inabainisha kuwa mtoto mmoja huzaliwa njiti kati ya kila watoto 10 duniani, na mmoja hufariki kila sekunde 40.

Hii ni changamoto ya kimataifa, lakini kwa Tanzania, suluhisho linapaswa kuwa la kitaifa, lenye dhamira ya kweli ya kisera, kibajeti na kiutekelezaji.

Serikali imeonyesha nia njema kupitia mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa kwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano hadi 40 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2025/26. Hili ni jambo la kupongeza. Lakini kufanikisha lengo hilo kunahitaji hatua thabiti zaidi, kuongeza bajeti ya afya, kuwekeza kwenye rasilimali watu na kuimarisha miundombinu ya huduma za watoto wachanga kuanzia ngazi ya wilaya.

Huu si wakati wa kuridhika na mafanikio tuliyonayo. Ni wakati wa kuongeza kasi ya jitihada. Tunaweza kuwa tumepunguza vifo vya watoto wachanga kwa zaidi ya asilimia 50 tangu mwaka 1990, lakini kila mtoto anayepoteza maisha kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika ni hasara kubwa kwa familia, jamii na taifa.

Serikali, wadau wa afya, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana kwa dhati kuhakikisha watoto wachanga wanapewa nafasi ya kuishi na kustawi. Hakuna taifa linaloweza kujenga uchumi imara bila kuwa na kizazi kilichoanza maisha yake kwa afya bora.

Ili kuimarisha mapambano haya, ni muhimu pia kuwekeza zaidi katika utoaji wa elimu kwa umma kuhusu maandalizi ya kupata na kumtunza mtoto mwenye afya bora. Elimu hii inapaswa kuwafikia wazazi, hasa wajawazito na wale wanaopanga kupata watoto, kuhusu umuhimu wa huduma za kabla na baada ya kujifungua, lishe bora, usafi wa mazingira, na dalili za hatari kwa mama na mtoto.

Elimu hii itasaidia kuondoa imani potofu zinazoweza kuchelewesha au kuzuia upatikanaji wa huduma stahiki. Changamoto hizi zisipuuzwe. Maisha ya mtoto mchanga si jambo la kusubiri. Ni lazima tutende sasa.