Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimepokea wanachama wapya 250 kutoka Jimbo la Kinondoni leo Jumapili, Julai 27, 2025 wakati chama hicho kilipofanya mkutano mkuu wa jimbo hilo.
Sera za chama, kushiriki uchaguzi, mabadiliko ni miongoni mwa sababu zilizofanya chama hicho kupokea wanachama wapya jimboni hapo kama alivyosema Katibu wa Jimbo la Kinondoni Chaumma, Amon Mwakasege.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu amesema hakina hiyana, ugomvi wala chuki na yeyote bali hasira za chama hicho zipo pale Watanzania wanapodhulumiwa haki zao.
“Chaumma hatuna shida na tunatamani tuwe daraja la kuunganisha vyama vyote. Sisi hatuna unyonge. Hatuna chuki, hasira zetu zipo pale Watanzania wanapocheleweshewa maendeleo yao,” amesema.
Amesema akitokea kiongozi yeyote wa upinzani anayewahamasisha Watanzania kupiga kura wao Chaumma hawana shida naye.
Akikabidhi kadi za uanachama wa chama hicho Mwalimu amesema jimbo la Kinondoni linapaswa kuelewa chama kinataka kushinda uchaguzi.
Amesema kiu ya Watanzania wanaoishi Kinondoni ni kuona maendeleo na mabadiliko kwa ujumla. Akieleza zaidi amesema Dar es Salaam inarudi kwenye mikono ya upinzani.

Viongozi na wanachama wa chama hicho waliokabidhiwa kadi za uanachama na Katibu Mkuu, wanatoka katika Kata za Makumbusho, Mzimuni, Tandale, Ndugumbi, Mwananyamala, Kijitonyama, Kinondoni, Makumbusho, Kigogo na Magomeni.
Mwenyekiti wa Chaumma Kinondoni, Rahimu Delenya amesema chama hicho kinataka kuiangusha CCM na kushika dola.
“Tukapige kura ya ukombozi tupate mabadiliko. Nafahamu matatizo ya watu wa Kinondoni ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana waliohitimu vyuo vikuu. Jimbo hili linaenda kuwa salama,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa wa Chaumma, Patrick Assenga amesema katika uchaguzi wa Oktoba wanachokwenda kukifanya ni kumalizana na CCM kwa kuiondoa madarakani.

Waliokabidhiwa kadi wafunguka
Zakim Mohammed kutoka kata ya Mwananyamala amesema anataka mabadiliko ndio maana ameamua kujiunga na chama hicho.
“Mabadiliko kwa vijana kama kupata kazi na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla,” amesema.
Mariam Khamis kutoka Kata ya Kigogo amesema anataka maendeleo ya Tanzania na mabadiliko ya kiuongozi ndio maana ameamua kuingia Chaumma.