Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Biteko leo ameongoza washiriki zaidi ya 12,000 wa mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma huku akiwapongeza waandaaji wa mbio hizo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kufanikiwa kukusanya fedha kiasi cha sh milioni 700 zitakazoelekezwa katika kufadhili malengo makuu matatu yenye dhima ya jumla ya kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Katika mbio hizo zilizohusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, ilishuhudiwa washiriki kutoka Tanzania, Kenya na Uganda wakichuana vikali kwa kuibuka washindi kwenye mbio tofauti hususani zile za km 10, km 21 na km 42. Dkt Biteko aliwaongoza viongozi mbalimbali wakiwemo wa kitaifa na viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali walioshiriki kwenye mbio za KM 5.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi na wadau mbalimbali wa mbio hizo, Dkt Biteko pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa mafanikio hayo, alionyesha kuguswa na ongezeko kubwa la washiriki wa mbio hizo kutoka washiriki 1,500 mwaka 2020 hadi kufikia washiriki 12,000 waliojiandikisha rasmi kushiriki mbio hizo mwaka huu.Hatua hiyo alisema inasadifu mwamko mkubwa wa wananchi kushiriki katika michezo hatua ambayo itasaidia katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa moyo, kisukari na figo.
“Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 33 ya Watanzania wanakabiliwa na changamoto ya uzito ulipitiliza huku asilimia 28 ya Watanzania wakikabiliwa na changamoto ya shinikizo la damu. Kwa takwimu hizo ukweli unabaki kuwa suala la mazoezi sio suala ya hiyari bali ni hitaji la lazima kwa mwili wa binadamu. Hii ndio sababu nawapongeza sana NBC na wadau wengine kwa jitihada zao za kubuni matukio ya michezo kama haya…hongereni sana,’’ alipongeza
Dkt Biteko alioumba uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuzitambua rasmi mbio za NBC Dodoma Marathon kama kivutio rasmi cha utalii na kichocheo cha Uchumi katika mkoa huo kutokana na mchango wake katika kutangaza utalii wa mkoa huo sambamba na uchocheaji wake Uchumi wa wananchi kupitia mzunguko wa fedha utokanao na idadi kubwa ya wageni wanaotembelea jiji hilo ili kushiriki mbio hizo.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof Paramagamba Kabudi pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kuwa mdau mkubwa wa sekta ya michezo hapa nchini kupitia jitihada zake mbalimbali, alisema ukubwa wa mashindano hayo ya NBC Dodoma Marathon unatoa fursa kwa mamlaka zinazosimamia mchezo huo kutumia washindi mbalimbali waliopatikana kwenye mbio hizo kuliwakilisha taifa kwenye mashindani mbalimbali ya kimataifa yakiwemo mashindano ya Olympics na yale ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw Theobald Sabi alisema kiasi cha mil 400 kati ya fedha zilikusanywa kupitia mbio hizo kitaelekezwa katika kufanikisha malengo ya mbio hizo ambayo ni kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200 pamoja na kuanzisha mpango mpya wa kufadhili masomo ya wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini.
Aidha Bw Sabi pamoja na Dkt Biteko walikabidhi hundi za fedha zilizotokana na mbio hizo ambapo kiasi cha Tsh mil 200 kilikabidhiwa kwa taasisi ya Benjamini Mkapa ili kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200, Fedha kiasi cha sh mil 100 kilikabidhiwa kwa taasisi ya Ocean Road ili kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kiasi cha mil 100 kilikabidhiwa kwa taasisi ya AMREF Health Africa kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini.
“Mafanikio haya yanachochewa na dhamira yetu kama benki ya kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii tunayoihudumia. Pia nawapongeza sana wadau mbalimbali waliojitokeza kufanikisha mbio hizo wakiwemo wadhamini wetu wakuu Kampuni ya GSM Group sambamba na wadhamini wengine muhimu ikiwemo Kampuni ya Bima ya Sanlam pamoja na wadhamini wengine wote waliotuunga mkono,’’ alisema.
Katika mbio hizo ilishuhudiwa Mwanariadha kutoka Kenya Moses Mengich akiibuka mshindi wa kwanza mbio za km 42 (Full Marathion) kwa upande wa wanaume baada ya kutumia muda wa saa 2:12:56 akifuatiwa na Mkenya mwezake Kipyeko Naman alietumia muda wa saa 2:13:25 huku kwa upande wa wanawake mbio hizo ilishuhudiwa Mwanaridha Joy Kemuma kutoka Kenya akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 2:31:57 akifuatiwa na Mkenya mwenzake Jacinta Chepkoech alietumia muda wasaa 2:33:56
Washindi wa kwanza hadi wa kumi kwenye mbio hizo wote walipatiwa zawadi ya fedha taslimu ambapo kwenye mbio za km 42 washindi wa kwanza waliondoka na zawadi ya fedha taslimu Tsh milioni 11.5 kwa jinsia zote huku washindi wa pili wakiondoka na Tsh Milioni 5 na vocha za manunuzi.
Kwa upande wa mbio za km 21 wanaume ilishuhudiwa Mwanariadha kutoka Tanzania, Felix Simbu akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 1:32:45 akifuatiwa na Mtanzania mwingine Boay Maganga alietumia muda wa saa 1:33:25 huku kwa upande wa wanawake mbio hizo ilishuhudiwa Hamida Mussa akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 1:48:52 akifuatiwa na Judith Cherono alietumia muda wa saa 1:49:00
Washindi wa kwanza kwenye mbio hizo za km 21 waliondoka na zawadi ya fedha taslimu Tsh milioni 5.5 kwa jinsia zote huku washindi wa pili wakiondoka na Tsh 2.5.
Pamoja na zawadi hizo za fedha taslimu zenye jumla ya sh mil 82, washindi hao waliweza kupata zawadi za vocha za manunuzi kutoka kwa wadhamini wa mbio hizo kampuni ya GSM Group aliyotoa zawadi za vocha ya manunuzi zenye thamani ya sh mil 4 kwa washindi wa mbio za KM 10 pamoja na kampuni ya Sketchers iliyotoa zawadi za vocha za manunuzi kwa washindi wa mbio za km 42 na km 21.
Naibu Waziri Mkuu Dkt Dotto Biteko (wa pili kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Tsh milioni 100 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Diwani Msemo (wa tatu kulia) iliyotolewa na Benki ya NBC kwa ajili ya kuchangia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika leo kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof Paramagamba Kabudi (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa pili kulia) Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw Emmanuel Tutuba (kulia) na viongozi wengine kutoka serikalini na wadau wa mbio hizo.
Naibu Waziri Mkuu Dkt Dotto Biteko (wa pili kushoto) akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa Amref Health Africa Tanzania, Dk. Florence Temu (katikati) mara baada ya kumkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Tsh milioni 100 iliyotolewa na Benki ya NBC kwa ajili ya kusaidia kuanzisha mpango mpya wa kufadhili masomo ya wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika leo kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof Paramagamba Kabudi (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa pili kulia) Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw Emmanuel Tutuba (kulia) na viongozi wengine kutoka serikalini na wadau wa mbio hizo.
Naibu Waziri Mkuu Dkt Dotto Biteko (wa tatu kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Tsh milioni 200 muwakilishi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation iliyotolewa na Benki ya NBC kwa ajili ya kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200 kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika leo kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (kushoto), Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof Paramagamba Kabudi (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa tatu kulia) na viongozi wengine kutoka serikalini na wadau wa mbio hizo.
Naibu Waziri Mkuu Dkt Dotto Biteko (wa pili kushoto) akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh mil 5.5 kwa mwanariadha wa kimataifa kutoka Tanzania, Alphonce Simbu alieibuka mshindi wa kwanza (kwa upande wa wanaume) wa mbio za km 21 za NBC Dodoma Marathon, zilizofanyika leo kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof Paramagamba Kabudi (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa kulia alievaa kofia) na viongozi wengine kutoka serikalini na wadau wa mbio hizo.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM Group, Mhandisi Hersi Said akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa mbio hizo. Kampuni ya GSM Group ndio mdhamini mkuu wa mbio hizo.
Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni ya Bima ya Sanlam Insurance Bw Mika Samwel akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa mbio hizo. Kampuni ya Bima ya Sanlam Insurance ni moja ya wadhamini muhimu wa mbio hizo.
Washikiri mbalimbali wa mbio za NBC Dodoma Marathon wakishiriki mbio hizo.