Haisaidii kumnyanyasa aliyezaa bila ya ndoa

Simulizi ya Recho, mama wa mtoto mmoja, niliyezungumza naye wiki iliyopita inawakilisha ugumu mkubwa wanaoupitia wanawake wengi wanaolea watoto peke yao.

Ingawa kumtunza mwanawe si jambo linalomsumbua, lakini upweke wa kihisia unaathiri vikali ustawi wa afya yake ya akili.

Hili linachangiwa na tabia ya jamii yetu kuwahukumu kwa kuwachukulia kama watu wasiostahili upendo wala ndoa kwa kosa la kuzaa bila ndoa.

Kwa nini, kwa mfano, wanaume wengi wanaogopa kuoa wanawake wenye watoto? Kubwa ni kujihesabia haki na kutokujisumbua kuelewa mazingira yanayowafanya wanawake wengi kuzaa bila ndoa.

Ukiangalia namna wanaume wanavyowakataa na kuwanyanyasa wanawake wenye watoto wao, unajiuliza, hivi kweli wao ndio wenye maadili zaidi? Kwa nini wanaume wengi mwenye watoto, tena na wanawake tofauti, wanaingia kwenye ndoa bila kubezwa kama inavyotokea kwa mwanamke mwenye mtoto?

Jingine ni dhana kuwa uhusiano wa kimapenzi na mwanaume aliyezaa naye huwa haukatiki. Hili linahitaji kutazamwa kwa jicho pana lisilo na lawama. Kwa nini, kwa mfano, mtu afike mahali pa kurudia matapishi yake mwenyewe?

Upweke unaweza kumfanya kweli mwanamke akawa mwathirika wa mwanaume mhuni anayetumia upweke wa mwanamke kumuumiza, kumwaacha, kumrudia na kumwacha. Ufumbuzi wake hauwezi kuwa lawama kwa mwanamke bali uhuni wa wanaume wanaopenda kuchezea hisia za wanawake hasa wanaopitia manyanyaso ya kihisia.

Pia kuna hili la hofu ya mwanaume kuona atalazimika kubeba ‘mzigo’ wa mtoto asiye wake. Ukitazama hofu hizi, kwa kiasi kikubwa, unaiona chuki ya jamii inayowakandamiza wanawake waliozaa, kuwafanya waonekane “wameharibikiwa”

Mitazamo kama hii, kwa kiasi kikubwa, inachochewa na watu wanaoaminika katika jamii, saa nyingine wanaojiita wacha Mungu, wanaopenda kujitangaza kwa ukamilifu unaowapa haki ya kujiona kuwa hawawezi kabisa kuvumilia makosa ya wengine.

Ukichanganya na fikra dume zinazotumia makosa ya mwanamke kumwadhibu, kumnyanyasa na kumfanya ajione mtumwa kwa mwanaume ambaye naye hali inakuwa mbaya zaidi na anayeumia, mara nyingi, anakuwa mwanamke.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa watu hujifunza kwa makosa yao. Maamuzi mengi ya maana kwenye maisha hufanyika kwenye nyakati za maumivu na machozi mengi.

Mifano iko mingi. Ingawa tunaweza kuwahukumu wanawake kama Recho kwa makosa yao ya ujanani, tusisahau nyakati ngumu zina nguvu ya kumbadilisha mtu. Mwanamke anayepitia kukataliwa ujauzito, mwanamke anayepitia hali ya kutengwa na familia kwa sababu ya ujauzito, ana nafasi kubwa ya kuwa mtu anayejitambua zaidi, wakati mwingine kuliko mwanamke anayejihesabu kuwa mkamilifu asiyekosea.

Tunayo mifano ya wanawake wengi inayothibitisha kuwa maadili ya mwanamke hayapimwi na mimba ya ujanani wala kuwa na mtoto. Watu hubadilika na hawatoi taarifa.

Hata kama kweli mtu aliwahi kuwa na tabia zisizofaa, tukumbuke nyakati hubadilisha watu. Kumhukumu mtu kwa makosa ya jana haikufanyi kuwa mtu bora kuliko yeye.

 Kabla ya kukutana na Adam, Recho alikuwa msichana aliyejitunza, akisoma chuoni na kufahamika kama mwanamke mwenye maadili. Kosa lake moja la kuuamini upendo wa wanaume matapeli kama Adam halipaswi kuamua mustakabali wa maisha yake yote.

Katika mazungumzo yetu nakumbuka Recho aliniambia, “Natamani kuwa na mwanaume atakayenipenda mimi na mtoto wangu, na ninaamini nina mengi ya kufanya kama mwanamke anayejitambua.”

Hili, kwa hakika, linaonesha kuwa Recho si tu hapaswa kuhukumiwa kwa ukali tofauti na wanawake wenzake waliofanya mengi lakini hawakupata watoto, lakini pia ana sifa za kuwa mwenzi bora.

Msichana kama Recho amedhihirisha kuwa na uwezo wa kushinda changamoto, akionyesha ustahimilivu na uwajibikaji. Pamoja na yote magumu aliyoyapitia, msongo wa mawazo na wakati mwingine kukata tamaa, bado ameweza kumtunza mtoto wake, Isaac.

Tukiacha mtazamo finyu wa kuwaona wanawake waliozaa bila ndoa kama tatizo, tukawapima kwa uwezo wao wa kujitambua, kuelewa wajibu wao katika familia, tunaweza kupunguza unyanyapaa dhidi yao na kuwasaidia kuponya majeraha yanayosababishwa na historia. zao na kuwapa nafasi ya pili ya kuendelea na maisha mengine kama wanawake wengine. Sioni namna gani tabia ya kuwanyanyasa wanawake waliozaa bila ndoa inatusaidia kujenga jamii bora yenye upendo na maadili.