KIUNGO wa Sisli Yeditepe, Shedrack Hebron amesema Ligi Kuu ya Uturuki itarejea mwezi wa 10, lakini mashindano mbalimbali anayoshiriki yatazidi kumweka fiti kwa ajili ya msimu mpya.
Hebron anacheza Ligi Kuu ya Uturuki pamoja na Watanzania wenzake, Ramadhan Chomelo wa Konya na Mudrick Mohamed anayekipiga Mersin.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hebron alisema kitendo cha kuibuka mfungaji bora kwenye mashindano ya Azam Amputee Football yaliyomalizika wiki iliyopita, kimemwongezea ushindani na kuwa fiti zaidi.
Mbali na mashindano hayo, lakini Septemba ataingia kambini na timu ya taifa kwa ajili ya kushiriki michuano ya Cecafa kwa walemavu yatakayofanyika Burundi.
“Tunakaa mapumziko muda mrefu, kwa hiyo ukipata nafasi ya kushiriki mashindano mbalimbali inakuwa bora zaidi kwa mchezaji mazoezi binafsi, pia yatazidi kuniweka imara msimu ujao,” alisema Hebron na kuongeza:
“Mashindano yale yalikuwa na faida nyingi, kubwa zaidi kwangu kuibuka mfungaji bora nikifunga mabao 14. Sikuwahi kuwa mfungaji kwenye maisha yangu ya soka, ni historia kwangu.”