Ilani ya ACT-Wazalendo kuja na majibu, kero za muda mrefu

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimesema Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni, imelenga kutoa majibu kwa changamoto zinazowakabili Watanzania.

Ilani hiyo itabeba mikakati thabiti ya kupambana na umaskini na kuondoa hali ya ufukara, ikiwa ni sehemu ya suluhu za kudumu kwa matatizo yanayowakumba Watanzania.

Licha ya changamoto ya umaskini, Watanzania wanakabiliwa pia na matatizo ya kilimo kisicho na tija, migogoro ya ardhi, ukosefu wa furaha, elimu isiyowafungulia fursa za maisha  na tatizo la ajira.

Makamu Mwenyekiti Bara ACT – Wazalendo, Isihaka Mchinjita akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.Picha na Michael Matemanga

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Julai 27, 2025, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita amesema chama hicho tayari kimefanya utafiti wa kutosha kuhusu hali ya Watanzania kupitia Ziara ya Operesheni Majimaji iliyofanyika kuanzia Julai mosi hadi 15, 2025.

Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kuongeza hamasa ya wananchi kuhusu umuhimu wa kura kupitia Kampeni ya ‘Linda Kura Oktoba.’

“Tunaamini katika kufanya tafiti huo, kabla ya kutoa sera. Bahati nzuri tumeshafanya hivyo na Ilani yetu ya uchaguzi itatoa majibu ya kina kwa changamoto hizo. Tayari baadhi ya sera zimeshatangazwa, kama ile ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo hasa wamachinga ambao kwa muda mrefu wamekosa mazingira ya kufanikisha shughuli zao,” amesema Mchinjita.

Ameeleza kuwa, kwa muda mrefu Watanzania wamekosa uongozi wa kuwajali kwa vitendo, huku akisema Serikali iliyopo imeshindwa kuandaa mipango ya maana ya kuwawezesha wananchi kuinuka kiuchumi na kufaidika na rasilimali za Taifa.

Akizungumzia kilimo, Mchinjita amesema ACT-Wazalendo inaamini ili sekta hiyo iwe na mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi, bajeti ya Serikali kwa kilimo, inapaswa kuongezwa kutoka asilimia tatu ya sasa na ifikie angalau asilimia 10.

“Inatakiwa tuwekeze kwenye kilimo cha kisasa chenye tija. Kwa sasa hakuna kilimo cha maana, hali inayoathiri maisha ya wakulima wetu,” amesema.

Akitolea mfano wa kilimo cha pamba, Mchinjita amesema kwa sasa hekta moja huzalisha kilo 250 tu, wakati nchini Benin, mkulima huyo huyo wa pamba huzalisha kati ya kilo 400 hadi 800 kwa hekta moja kutokana na uwekezaji mkubwa katika teknolojia na pembejeo za kisasa unaofanywa na Serikali yao.

“Hili ndilo linatufanya tuendelee kubaki nyuma. Wenzetu wanapiga hatua kwa sababu ya mipango madhubuti ya Serikali zao kuwasaidia wakulima,” amesema.

Pia, ametoa mfano mwingine wa chai, akisema wakulima wa chai Tanzania huuza kwa bei ya chini ukilinganisha na wenzao wa Kenya, licha ya wote kuwa katika ukanda mmoja wa Afrika Mashariki.

“Wakulima wa Kenya wanalindwa na mipango bora ya kuwatafutia masoko, tofauti na Tanzania ambako mkulima anapata asilimia 10 tu ya bei ya soko la dunia, ilhali jirani yake Kenya anapata hadi asilimia 60,” amesema.

Kuhusu suala la kuondoa umaskini, Mchinjita amesema ACT-Wazalendo imelenga kuchukua hatua za haraka na za muda mfupi kuinua kipato cha wananchi na kuendeleza shughuli za kiuchumi, hasa zile zinazohusu uzalishaji.

Amesema kupitia Ilani ya uchaguzi, chama hicho kimepanga kuweka mikakati ya muda mrefu itakayosaidia kuinua hali ya maisha na makazi ya Watanzania, kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 9(i) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mchinjita amesema changamoto hizo ndizo zinazowatia moyo zaidi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 ili kuhakikisha wanapata wawakilishi wanaoweza kutetea masilahi ya wananchi ndani ya vyombo vya uamuzi hasa Bunge.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Shangwe Ayo amesema Operesheni Majimaji katika awamu ya sasa iligawanyika makundi mawili.

Makamu Mwenyekiti Bara ACT – Wazalendo, Isihaka Mchinjita akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.Picha na Michael Matemanga

Amesema kundi la kwanza liliongozwa na kiongozi wa chama, Dorothy Semu aliyeambatana na Makamu Mwenyekiti Bara, Isihaka Mchinjita na watumishi wengine wa chama.

“Kundi la pili liliongozwa na kiongozi mstaafu wa chama, Ndugu Zitto Kabwe, akifuatana na Naibu Katibu Mkuu wa Bara, Esther Thomas pamoja na viongozi wengine, wanachama na watumishi wa chama,” amesema Shangwe.

Amesema kupitia ziara hiyo, Operesheni Majimaji imefanikiwa kufika moja kwa moja katika mikoa ya Kigoma, Simiyu, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Mtwara, Lindi na Pwani.

“Katika mikoa hiyo, chama kimeweza kung’amua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, kutoa msimamo wake kuhusu matatizo hayo, kueleza dhamira ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, pamoja na kuendelea na ujenzi na maandalizi ya chama kuelekea uchaguzi huo Oktoba,” amefafanua.