Dodoma. Wakati Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikiwataka wanasiasa na wafuasi wao kufanya kampeni za kistaarabu, baadhi ya vyama vya siasa vimetaka ofisi za tume hiyo kuwa wazi kabla na baada ya uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba uteuzi.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa mkutano wa kitaifa wa tume hiyo na vyama vya siasa kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele wakati wa mkutano wa kitaifa wa tume hiyo na vyama vya siasa kuhusu Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Kikao hicho kimefanyika baada INEC kutangaza ratiba ya uchaguzi mkuu, inayoonesha kuanzia Agosti 9-27, 2025 itakuwa utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea urais na makamu.
Agosti 14-27, utoaji fomu za uteuzi wa ubunge na madiwani, Agosti 27 ni uteuzi wa wagombea udiwani, ubunge, Rais na makamu wa Rais. Kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 ni kampeni za uchaguzi huo na Jumatano ya Oktoba 29 ni siku ya kupiga kura.
Pia, tume ilitangaza majimbo 272 kati ya hayo 222 yapo Tanzania Bara na 50 yapo Zanzibar yatakayoshiriki katika uchaguzi mkuu baada ya ongezeko la majimbo manane.
Pia, kata 3,960 zitafanya uchaguzi wa madiwani ikiwa ni ongezeko la kata tano.

baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchin wakiwa katika mkutano ulioandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Katika kikao hicho kilichofanyika leo Julai 27, 2025, Jaji Mwambegele amesema kipindi cha kampeni kunakuwa na joto kali la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa hali inayoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.
“Napenda kutoa rai kwenu na wafuasi wenu kwa kuwasihi kufanya kampeni za kistaarabu na hivyo kuepuka kufanya vitendo vitakavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi yetu,” amesema.
Jaji Mwambegele amesema tume itaendelea kuwashirikisha kwa kadri itakavyowezekana na kama kawaida itasimamia uchaguzi huu kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa uchaguzi.
Jaji Mwambegele amesema lengo ni kuhakikisha uchaguzi mkuu unakuwa huru, wa uwazi, wa haki na wa kuaminika kwa kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea na vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki.
Akiwasilisha mada, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima amesema katika uchaguzi huo kwa mara ya kwanza wafungwa na mahabusu watapiga kura ya urais pekee.
Pia, amesema itakapotokea wagombea watakapojitoa na kubakia mmoja, siku moja hadi tatu kabla ya uchaguzi, tume inaweza kupeleka mbele uchaguzi ili kuipa nafasi kuandaa upya karatasi za kupiga kura.
“Ofisi za wasimamizi wa uchaguzi zitakuwa wazi wakati wote katika uchaguzi, wagombea mnaweza kuleta fomu zenu tukazikagua kabla ya siku ya urejeshaji, hatutaki mtu ambaye anasifa za kugombea kukosa,” amesema.
Pia, amesema kwa upande wa majina ya wabunge na madiwani wa viti maalumu, yanatakiwa kupelekwa mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu.
Kuhusu maandalizi ya vifaa, Kailima amesema yanaendelea vizuri, “tunatarajia vifaa vyote vya uchaguzi vitapokewa na kusambazwa katika maeneo yote kwa wakati.”

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema tangu mwaka 1995, sasa itakuwa mara ya kwanza kupata daftari mwezi mmoja kabla ya uchaguzi.
Hata hivyo, Profesa Lipumba ameshauri mawakala waapishwe katika kata zao ili kurahisisha shughuli hiyo na kuwezesha mawakala wote kuapishwa.
“Mwaka 2015 uchaguzi ulikuwa ni bora kuliko wa mwaka 2020 ambao wewe ulikuwa mkurugenzi (Kailima) na sasa hivi wewe pia ni mkurugenzi,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha ADA-Tadea, Juma Ali Khatib amesema wamefanya kazi kwa uaminifu na kuwashirikisha wadau wote wa vyama vya siasa ambao wameridhika na namna ambavyo mchakato wa uchaguzi unavyoendelea.
“Siku ya urejeshaji wa fomu za wagombea ubunge, umesema kuwa ofisi hazitafungwa, wakati wa urejeshaji wa fomu, hicho kilikuwa ni kilio kikubwa kwa wagombea, wanafika muhusika hayupo hasa siku ile ya mwisho,” amesema.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Haji Ambari Hamis amehoji kura zitakazopigwa na wafungwa magerezani zitalindwa na nani hasa ukinzingatia kwa mgombea, kura moja ni mali.
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema wamejiridhisha kwenye orodha ya wasimamizi wa uchaguzi suala la wasimamizi kutokuwa makada wa vyama vya siasa, limezingatiwa.
“Naomba uchunguzi huo uendelee hadi chini, kuhakikisha wale wa chini sio wanachama wa vyama vya siasa na hata mkigundua baadaye muwatoe,” amesema.
Kuhusu hoja ya kuenguliwa kwa wagombea kwenye uchaguzi, Shaibu amepongeza suala la kuwekwa kwa siku tatu za INEC kukagua fomu za wagombea, lakini akataka kigezo cha kuenguliwa kwa mgombea kutokana na kasoro ya fomu kiondolewe na badala yake iwe ni sababu za Kikatiba tu.
Pia, ameshauri nakala za fomu ya matokeo ziwepo za kutosha na udhibiti wa karatasi za wapigakura ili kuepusha karasi feki za kupigia kura kwenye uchaguzi huo.
Katibu Mkuu wa TLP, Yustas Rwamugira ameshauri ijulikane viwango vya gharama vya malipo ya kiapo cha mgombea katika Mahakama kwa kuwa zimekuwa zikitofautiana.
“Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, hawa watu TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), ukibandika bango ukutani wanakuletea taarifa ulipie bango. Tunaomba na hili mtusaidie,”amesema Rwamugira.
Pia, ameshauri kuangaliwa kwa suala la viwanja kutokana na vingi kubadilishwa matumizi hasa mijini.
Katibu Mkuu wa AAFP, Rashid Rai ameshauri vyombo vya habari kutoa kipaumbele katika vyama vyote na si uegemea kwenye vyama vikubwa pekee.
Pia, ameomba kuwepo kwa mgawanyo wa vyombo vya habari vya ‘online’ kulingana na vyama vinavyofanya mikutano kwa sababu baadhi ya vyama havina uwezo wa kulipa gharama za mwandishi mmoja wa habari.
Katika uchaguzi huo, INEC imetangaza jumla ya watu milioni 37.65 wamejiandikisha katika uchaguzi mkuu huo, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025.