Ni ngumu na kamwe sio rahisi kumbadilisha mtu mwenye tabia ngumu awe rafiki. Mabadiliko haya yanawezekana ikiwa mhusika (mwenye tabia ngumu) atadhamiria na kuwa tayari kushughulika ili kubadilika.
Kwa hiyo kama ni ngumu au haiwezekani kumbadilisha, basi jaribu kubadili mtazamo wako na jinsi unavyoishi naye au nao, kwa sababu mara nyingi wewe ndio unayekwazika au kuumizwa wakati yeye (yule anayekuudhi) anafanikiwa na anaendelea na furaha zake tu.
Mawasiliano baina yetu na watu wengine yanajumuisha jinsi tunavyowafanyia wengine na jinsi wao wanavyotufanyia.
Kwa kubadili jinsi sisi tunavyowatendea wengine inaweza kubadili jinsi wao wanavyotutendea sisi. Hata kama ni kwa muda au kitambo kidogo tu. Hata kama hali hii haibadili hali kwa kudumu ila inaweza kurahisisha mazingira ya kuishi na mtu au watu wenye tabia ngumu.
Kila wakati lazima uwe na akili sana katika kuishi na watu wenye tabia ngumu, kama hutoweza kujizuia, na ukaanza kuwabwatukia basi itakuwa unaleta tatizo hasa pale ambapo mwenye tabia hii ngumu ni bosi wako. Je, utaropoka au kutukana kama ulivyozoea?
Hata kama mtu au watu wenye tabia hii wako ndani ya familia na yamkini ni wadogo kwako kiumri, bado kuropoka na kuwapayukia sio suluhisho, hali hii inaweza kukugharimu.
Najua kila mmoja wetu ana jinsi anavyofanya kwa mtu au watu wenye tabia ngumu. Wote hatuna namna moja, mmoja anaweza kuwa ni mkimya na mwenye ujasiri hata anapoudhiwa, mwingine hupayuka na kumjibu yule anayemuudhi.
Mwingine anaamua kulia tu anapoudhiwa, wako wanaozira na kuamua kutozungumza tena na aliyewaudhi, wapo ambao husambaza habari mbaya kuhusu huyo mwenye maudhi, wako ambao huamua kumwambia uso kwa uso jinsi walivyo kwazika, sijui staili yako ni ipi.
Ni rahisi sana kuumizwa au kuudhiwa na maneno au matendo ya mwingine, na mara mtu huyo anapojua kuwa unaumia, yeye hupata nguvu, hii huwa ndio silaha yake muhimu pale mnapopambana.
Unachotakiwa kufanya ni kuwaachia wakati wote wao wawe washindi, kamwe usitafute kushindana nao, utaumia mwenyewe.
Njia pekee ni kujitahidi kuwa mjanja na mwenye akili kuliko yeye na pia kuwa na ushawishi katika yale wanayotaka kuyatenda hata pasipo wao kugundua.
Unawajibu vipi watu hawa?
Ni jambo jema kuanza kujitazama jinsi unavyowatendea wengine na jinsi tunavyoshughulika na wale wanaotukwaza.
Kumbuka kuwa jinsi unavyoikabili hali katika mazingira fulani inawezekana isiwe hivyo katika mazingira mengine.
Watu wenye tabia ngumu na zinazotatiza mara nyingi huweka mitego ya maneno au matendo na kwa kiasi kikubwa unaweza kunaswa na kuwaruhusu wakuchezee jinsi watakavyo, na kati ya vitu wanavyo vipenda na kuvitamani ni kukuona unalia na kuumia na kuchanganyikiwa. Kwahiyo fikiri kwanza kabla hujafanya chochote mbele yao.Watu wa tabia hii mara zote huwachukulia na kuwatendea watu wote sawa kwa hiyo usifikiri kila alichosema au alichofanya kwako ni cha kibinafsi sana na alikikusudia kwako.
Angeweza kufanya au kusema hivyo hivyo hata kwa mwingine aliye karibu naye wakati ule. Kwa kufahamu hili itakusaidia kupunguza maumivu yanayoletwa na hisia zako kwake.
Hebu jiulize ni jinsi gani umewahi kukabiliana na mtu au watu wa jinsi hii, na je, ilikuwa ni kwa jinsi ya kuumiza au kuelemisha?
Fahamu kwamba kujibu kwa kupayuka, kutukana au kubishana haisaidii, bali kunakushusha chini ya miguu ya yule aliyekusababishia maumivu hayo, na sasa atakuwa anafurahia na kukuona wewe mjinga. Ni chaguo lako jinsi gani utakabiliana na mtu au watu wa aina hii, ingawa unaweza kuchagua njia bora itakayoweza kukusaidia kukuimarisha na kupunguza udhaifu wako, zaidi ya kuamua kuchagua njia ambayo itakuacha umeumia, umechoka, umekatishwa tamaa na umejeruhika moyo.
Hii haimaanishi uwe mtu wa kusema ndiyo tu kwa kila kitu na kila mtu, na haimaanishi kuwa hutakiwi kukasirika. Hapana! Hasira ni asili na haina tatizo lolote hapa, ila tu matokeo ya hasira hiyo ndiyo yanayoweza kuleta shida.
Je, ni jinsi gani unakabiliana na hasira yako na unaionyeshaje? Kwa fujo, kupayuka kubishana, kulia, kuvunja vitu, kunyamaza au…