Kwa mwanaume miezi mitano hii inatosha kubadili gia

Tuanze na kuambiana jambo moja: ‘Bado tuna nafasi’ na hii sio sentensi ya kutiana moyo kwa maneno matupu, ni ukweli wa maisha.

Bila kujali kama ulianza mwaka huu na malengo makubwa ukashindwa kuyatekeleza, au kama hujaona dalili ya kuyatimiza mpaka sasa, nataka ukumbuke bado hujachelewa.

Kila mwanaume amewahi kupitia wakati kama huo. Umeandika malengo, unaapa kubadilika, unasema mwaka huu wangu. Mwaka huu najenga. Mwaka huu nanunua gari. Mwaka huu nakuwa karibu na familia yangu zaidi.

Lakini miezi ikasonga, maisha yakatupiga kikumbo, nidhamu inayeyuka, na ukajikuta umerudi tena palepale unapopachukia. Dunia imejaa presha: presha ya mafanikio, presha ya kuwa baba bora, mume bora, kijana anayekimbiza maisha.

Lakini wakati mwingine, presha hiyo hiyo inatufanya tuone kama hatufai, kama hatuendi popote, kama tunaanguka kila siku. Lakini ukweli ni huu: kuanguka si mwisho wa safari, bali ni sehemu ya safari. Na uzuri ni kwamba, ukiona umeanguka maana yake ndiyo umeshaanza safari hivyo. Yaani uko pazuri.

Leo ni Julai. Tuna zaidi ya miezi mitano kabla mwaka haujaisha. Miezi mitano inaweza kubadilisha maisha yako kama utaamua? Unaweza kuacha pombe leo, na ifikapo Disemba uwe tayari umepona kabisa.

Unaweza kuanza kuweka akiba leo, na ikifika mwisho wa mwaka uwe na hela ya maana. Miezi mitano ni mingi kaka. Miezi mitano inatosha kufanya jambo lolote ambalo linakutisha ukiitumia vizuri.

Usiseme tena, “nitasubiri Januari.” Hapana. Januari ni tarehe tu. Haitabadilisha maisha yako, ni wewe peke yako unaweza kufanya hivyo. Na ikitokea unaona unajisikia kuisubiri Januari sana nataka ujiambie, ikifika hiyo Janauri nitafanya nini? Kisha ukipata jibu jiulize, kwanini nisifanye sasa hivi?

Pia punguza kujilinganisha na wanaume wengine. Hujui wanapitia nini. Wengine wanaonekana wana mafanikio, lakini hawana amani. Wengine wanaonekana wamepotea, lakini moyoni wameanza safari mpya ya kubadilika.

Kila mtu alipanga malengo yake na mipango yake mwanzo wa mwaka akiwa mwenyewe chumbani.  Hukuwapo kama wao ambavyo hawakuwapo wakati unapanga mipango, kwahiyo wewe jielekeze kwenye maisha yako na mipango yako.

Halafu Disemba haipaswi kuwa kioo. Haipaswi kuwa mwezi wa kujilaumu. Inapaswa kuwa mwezi wa kutazama nyuma na kusema.

“Nilijitahidi.” Na hata kama itatokea hujatimiza malengo, basi angalau ujivunie hatua ndogo ulizozianza.

Kwa kifupi bao una miezi mitano ya kuandika hadithi mpya. Na hata ikifika Disemba hujafika unakotaka, bado kuna Disemba kibao ziko mbele.

Unapanga tena, unachukua hatua za dhati, amini kwamba kuna Disemba moja itakuwa ya kipekee.

Usikubali kuwa mfungwa wa tarehe. Usikubali uone mwaka unaisha bila kuona mabadiliko.  Wewe anza kubadilika muda huu utashangaa jinsi miezi mitano iliyobaki inavyokuwa ya ushindi kwako.