Malezi ya mtoto huakisi mwelekeo wa wazazi

Ili kuunda familia yenye msingi imara wa heshima na maadili mbele ya jamii, wazazi wanapaswa kufanya kazi ya ziada katika kulea watoto wao kwa hekima, uvumilivu na maombi.

Tafiti za wataalamu wa saikolojia wa malezi zinaonyesha msisitizo kuwa watoto wadogo ni wadadisi, wanaopenda kujifunza kwa kuangalia na kuiga kila wanachokiona.

Wanapojifunza kupitia matendo ya watu wazima walioko karibu nao, basi watoto hao huakisi kile wanachoona, kiwe chema au kibaya. Mtaalamu mmoja wa saikolojia, Julius Mpambilyoto nilipozungumza naye juu ya hili, aliniambia kuwa hii inawaweka wazazi katika nafasi muhimu ya kuwa mfano bora kila wakati.

Anasema pamoja na ujuzi wa kimalezi, wazazi wanapaswa kumtanguliza Mungu katika kila hatua ya kulea mtoto.

Kwa maana nyingine, hii inamaanisha kuwa malezi yanayojengwa juu ya msingi wa kiroho, hujenga watoto wenye hofu ya Mungu, wanaotambua thamani ya wema, upendo na uadilifu.

Kwa kauli hiyo, naweza kusema kuwa maneno ya wazazi yana nguvu kubwa ambayo inaweza kumjenga au kumbomoa mtoto.

Yaani baraka na maneno ya kutia moyo huwajenga watoto kisaikolojia huku maneno ya kejeli na laana yanweza kuwa chanzo cha maumivu na mkanganyiko mkubwa maishani mwao.

Methali ya Kiswahili isemayo “Mwana umleavyo ndivyo akuavyo” inathibitisha kuwa tabia ya mtu mzima hujengwa tangu utotoni.

Hata hivyo, si malezi ya amri na hofu tu yanayoweza kumwelekeza mtoto. Wazazi wengi huweka sheria kali bila kuelewa kuwa hatua hiyo inaweza kumtia mtoto katika hofu au uasi wa kimyakimya.

Malezi ya namna hiyo huwafanya watoto kutamani uhuru wa nje ya nyumba, hali ambayo inaweza kuwa hatari zaidi kwa maendeleo yake.

Malezi bora hujikita kwenye uelewa, upendo, mawasiliano ya wazi na kushirikisha mtoto katika uamuzi mdogo mdogo unaomgusa. Mtoto anahitaji kuhisi kuwa anasikilizwa, anaeleweka na anathaminiwa.

Katika zama hizi za maendeleo ya kisayansi na kijamii, malezi si tu kumpatia mtoto chakula, mavazi na elimu, bali pia ni pamoja na kumwandaa kitaaluma na kimaadili kwa maisha ya baadaye.

Kazi ya kulea haianzi pale mtoto anapozaliwa. Wataalamu wanasema wazazi wanapaswa kuanza kuzungumza na mtoto tangu akiwa tumboni, ili ajifunze kutambua sauti zao. Mazungumzo haya ya mapema humsaidia mtoto kuanza kujenga uhusiano wa karibu na wazazi wake.

Wanasema hiyo inaweza kumjengea msingi mzuri wa kihisia na kiakili atakapozaliwa. Ila swali la msingi ni je, wazazi wa leo wanafahamu dhima yao katika ulinzi na makuzi ya watoto wao?

Katika jamii ya sasa, majukumu mengi ya kulea yamehamishiwa kwa walimu shuleni na wasaidizi wa kazi za nyumbani, hali ambayo hupunguza ushiriki wa wazazi katika maisha ya kila siku ya watoto wao.

Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wazazi wakijitetea kuwa hawana muda wa kukaa na watoto kwa sababu ya shughuli nyingi za kutafuta riziki.

Ingawa maisha ya sasa yanahitaji juhudi kubwa ya kujikimu, hoja hiyo haiwezi kuwa sababu ya kutoshiriki kikamilifu katika malezi.

Mzazi anayemfuatilia mtoto wake kwa karibu kila siku, humsaidia kumwepusha na mambo maovu kama unyanyasaji na maovu yanayoweza kumpata nje au hata nyumbani.

Mtoto anayelelewa kwa upendo, uangalizi, maadili na maombi, anayo nafasi kubwa ya kukua katika mazingira salama yakayomjenga aje kuwa raia mwema mwenye mchango chanya kwa jamii.

Lakini mtoto anayekosa ulinzi wa karibu wa wazazi wake, yuko katika hatari kubwa ya kuathiriwa na ukatili, mmomonyoko wa maadili na vishawishi vinavyoweza kumwingiza katika makundi mabaya.

Hivyo basi, huu ni wakati wa wazazi na walezi kujitathmini upya na kuhakikisha wanabeba wajibu wao ipasavyo.

Malezi bora huzaa watoto wenye nidhamu, maadili na heshima ambao wakiwekwa mbele ya watu, wanatambulika kwa mwenendo wao mzuri.

Tukifanya hivi kwa dhati, tutapunguza kwa kiasi kikubwa vilio vya mmomonyoko wa maadili vinavyoikumba jamii yetu sasa.

Watoto wetu si tu furaha ya familia, bali pia ndio msingi wa taifa bora la kesho. Kila mzazi ana nafasi ya kipekee ya kujenga taifa hilo kupitia malezi sahihi ya mtoto wake.