Malezi yanavyotutoa kutoka kuwa watu kuwa vitu

Jana nimekutana na Zaynab kwenye kibaraza cha urojo mjini Zanzibar. Zaynab, mama wa watoto wawili, alikuwa amekuja na watoto wake kwa matembezi, lakini kitu kilichonishangaza ni kwamba muda wote watoto walikuwa wameinamia simu zao, kila mmoja na yake, wakiangalia katuni na kucheka, na hapakuwa na mazungumzo.

“Imekuwaje Zaynab akaja na watoto lakini hawazungumzi? Kwa nini watoto wamekuwa na uraibu kiasi hiki?” nikajiuliza. Nilipochokoza mazungumzo Zaynab alijitetea, “Maisha ni magumu. Ninawapa simu ili niweze kumudu mambo yangu.”

Wazazi wengi hatuishi maisha tofauti na haya ya Zaynab. Tunatumia vitu kama mbadala wa uwepo wetu kwenye maisha ya watoto.

Hata kubwa ni kwamba simu inaweza kuwafurahisha kwa muda, lakini haizibi pengo la kukosa kitu muhimu kwenye maisha.

Mtoto, kimaumbile, anahitaji uhusiano halisi na watu wake wa karibu, aonekane, asikike, aeleweke, athaminike. Hili lisipotokea hali ya upweke kuanza kuwasumbua watoto.

Pengo hili linaweza kuathiri ukuaji wao wa kihisia. Watoto wanaokuzwa na skrini wanaweza kushindwa kujifunza jinsi ya kushughulikia hisia zao. Wanaweza kuwa na hasira zilizofichika au kujifunza kuwa simu ndiyo suluhisho la kila changamoto.

Tunaambiwa, kitalaamu, watoto wanaozoea vitu kuliko watu wanakosa stadi za maisha, kama kushirikiana na watu, kuelewa hisia za watu, kuonesha huruma, kwa vile wanakuwa wamezoea kucheza na simu badala ya watu.

Hii inaweza kuwafanya wajisikie kutengwa, na baadaye maishani, wanaweza kupata changamoto katika kujenga mahusiano ya maana.

Kwa nini watoto wa Zaynab wamezoea simu kupindukia? Kwanza, maisha ya Zaynab ni pilikapilika. Alisema, “Mimi ni mama wa pekee, nafanya kazi zinazochukua muda wangu mwingi. Narudi nyumbani nikiwa taabani. Simu inasaidia kuwanyamazisha watoto ili niweze kufanya mambo yangu.” Maisha ya sasa yanawafanya wazazi kama Zaynab wawe bize kila siku, wakitafuta pesa za kumudu chakula, ada, na mahitaji mengine. Muda wa kukaa na watoto unapungua, na simu inakuwa kama kishikwambi cha kihisia—mtoto akilia, unawasha katuni; akiwa na wasiwasi, unampa mchezo wa kidijitali.

Pili, teknolojia imeingia kila kona ya jamii yetu. Simu ziko kila mahali, na watoto wanakua wakiwa wamezungukwa na skrini. Zaynab alisema, “Hata kama sitaki, wenzao wote wana simu, na watoto wangu wanahisi wameachwa.” Jamii yetu imebadilika—kufanikiwa siku hizi kunamaanisha kumudu vitu vya kisasa, na simu inaonekana kama kielelezo cha mafanikio.

Changamoto yake ni kwamba watoto wanajifunza kuwa skrini zinaweza kuchukua nafasi ya watu, na hii inawapunguzia uwezo wa kuhusiana kihisia.

Pia kuna hili la shinikizo la kijamii. Wazazi wanahisi wanapaswa kuwapa watoto wao kila kitu wanachotaka ili waonekane wanafaa. Shinikizo hili linawafanya wazazi wafikiri kumpenda mtoto maana yake ni kumpa vitu, hali inayowafundisha kuthamini vitu kuliko watu halisi.

Zaynab anatetea msimamo wake, “Bila simu, watoto wangekuwa wakilia na sina la kufanya maana nakuwa nimechoka. Siwezi kabisa kushughulika nao kila wakati. Inachosha.” Je, Zaynab, pamoja na kuchoshwa na shughuli nyingi, anaweza kuweka dakika chache za kuhusiana na watoto bila simu na vishikwambi? Alifikiri, kisha akasema, “Lakini wao wanapenda katuni, na mimi niko bize. Sijui kama inawezekana.”

 Ingawa Zaynab ana sababu za msingi za kutoongea na watoto, bado sababu hizo haziondoi hitaji la kisaikolojia la mtoto kuonekana, kusikilizwa na kueleweka ili ajisikie salama.

 Tunaweza kujitetea kwa kuwa na shughuli nyingi lakini watoto hawatakumbuka kuwa tulikuwa na shughuli nyingi. Kitakachokumbukwa zaidi na watoto ni kile kilichochukua nafasi ya ombwe la kuonekana, kusikilizwa na kueleweka.

Je, Zaynab anaweza kuweka ratiba, kama kupata chakula cha jioni pamoja na watoto bila simu, au kuwa na utamaduni wa hadithi fupi kabla ya kulala? “Hilo linaweza kulifanya kazi, ingawa kiukweli bado naona simu ndio njia rahisi zaidi.

Ninachojifunza kwa mazungumzo haya ni kwamba upendo wa mama haubadilishwi na kitu chochote. Nisipojaribu kuwapa muda wangu, nitawafundisha kuishi maisha yao bila kunitegemea. Wataanza kuamini vitu vina thamani kuliko watu na hiyo itakuwa hatari.”

Zaynab anapambana kuwapa watoto wake kila kitu wanachokihitaji, lakini simu zinazochukua nafasi ya upendo zinaacha pengo kubwa. Kuna tunalojifunza hapa. Kwanza, upendo wa kihisia ni muhimu zaidi kuliko vitu.

Hata kama uko bize, dakika chache za kusikiliza mtoto wako zinaweza kujaza pengo ambalo skrini haiwezi kulijaza. Pili, ili watoto wasizoee vitu kupindukia, tuna kibarua kigumu cha kutafsiri upya maana hasa ya maisha.

Usipomsaidia mtoto kuelewa thamani ya uso wa mtu, thamani ya kuzungumza na mtu, thamani ya kusikilizwa na mtu, thamani ya kueleweka na mtu, unamfundisha kuwa vitu ni muhimu kuliko watu.

Ikifikia hapo unakuwa umewahamisha kutoka kuwa watu hadi kuwa vitu. Inakuwa hatari kubwa.