Musoma. Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mara wameziomba mamlaka husika kuanzisha mchakato wa kupatikana kwa alama au nembo ya mkoa huo itakayokuwa utambulisho rasmi kama ilivyo mikoa mingine.
Tofauti na mikoa mingine, Mkoa wa Mara hadi sasa hauna nembo kama ilivyo Mwanza, Arusha, Dodoma na Dar es Salaam.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumapili Julai 27, 2025, wamesema vipo vitu vingi ikiwamo rasilimali zilizomo ndani ya mkoa huo zinazoweza kutumika kuweka alama ya mkoa kama madini, mazao ya uvuvi ndani ya Ziwa Victoria, kilimo na ufugaji.
“Mimi napendekeza ijengwe sanamu nzuri na ya kisasa ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere pale Ziroziro kwa sababu hakuna sanamu yake ndani ya mkoa tofauti na mikoa mingine. Pia, Baba wa Taifa anatokea Mara, kwa hiyo mbali na kuwa itakuwa alama ya mkoa, tutakuwa tunamuenzi,” amesema Mtatiro Chacha.
Chacha amesema umefika wakati mkoa huo na wilaya zake kuwa na alama maalumu ya kuutambulisha tofauti na ilivyo sasa.
Amesema maeneo ya mizunguko ya barabara yapo wazi bila alama zozote.
“Tuwe na kitu kinachotambulisha kuwa hapa ni Mara, na kitu hicho kitokane na vile vitu tulivyonavyo hapa kwetu, mbali na Nyerere, tuna samaki, wanyama, madini na vitu vingi vizuri tu,” amesema Rehema Nyamoko.

Kwa upande wake, John Chibasa amesema uwepo wa alama hizo pia utasaidia kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa watu kuwa wakazi wa Mkoa wa Mara ni wakatili na sio wakarimu.
“Huko nje watu wanaamini kuwa sisi ni wakatili na sio wakarimu, kuna dhana imejengeka kuwa hata vibao vyetu vimeandikwa kwa upekee, eti ‘Sasa unaingia Mara’ kitu ambacho hakipo. Ili kuondoa dhana hii, wahusika waweke alama nzuri kuonesha yale mazuri yaliyopo kwenye mkoa wetu,” amesema Chibasa.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema wilaya yake ipo katika mchakato wa kuweka nembo ya mkoa katika wilaya yake ambayo ndio makao makuu ya mkoa.
Amesema mbali na nembo hiyo, pia, wanatarajia kujenga na kuboresha bustani maarufu iliyopo katikati ya mji wa Musoma maarufu Bustani ya Malkia Elizabeth na itatumika kwa ajili ya uwekezaji, hivyo kuwa chanzo cha mapato kwa halmashauri.

“Yapo mengi tumepanga na tayari mchakato umeanza, pamoja na mambo mengine tunatarajia kuweka runinga katika mzunguko uliopo ndani ya manispaa yetu itakayokuwa ikionesha vivutio vya uwekezaji na uchumi ikiwamo utalii uliomo ndani ya mkoa sambamba na miradi ambayo imetekelezwa na ile inayoendelea kutekelezwa,” amesema Chikoka.
Amefafanua kuwa, tayari mchoro umeandaliwa kuonesha namna vitu hivyo vitakavyojengwa na kuufanya mji huo kuvutia zaidi na kuwa msafi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Akisisitiza kuhusu jambo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema mkoa uko kwenye mchakato wa kupata nembo au alama hiyo.
Amesema tayari wamepokea mapendekezo mengi kutoka kwa wadau mbalimbali wakipendekeza alama gani kuweka pamoja na eneo la kuweka alama hiyo.
“Tunafanya uchambuzi sasa, mapendekezo ni mengi wapo wanaopendekeza sanamu ya Mwalimu Nyerere, madini, mifugo, ziwa, samaki na Hifadhi ya Serengeti na mapendekezo yote ni mazuri, hivyo uchambuzi unafanyika ili tuamue tutumie nini na kwa namna gani,” amesema Kanali Mtambi.