Mbeya City kumrejesha Kigonya Bara

UONGOZI wa Mbeya City uko katika mazungumzo ya kumrudisha tena Tanzania aliyekuwa kipa wa Azam FC, Mganda Mathias ‘Kone’ Kigonya, baada ya nyota huyo kumaliza mkataba wake na Yadah Stars FC ya Harare, Zimbabwe aliyojiunga nayo Julai 4, 2024.

Kigonya aliyezaliwa Februari 2, 1996, katika Mji wa Lyantonde huko kwao Uganda, inadaiwa yupo katika mazungumzo na timu hiyo na kwa sasa inajipanga kuhakikisha inapata wachezaji wakubwa na wenye uzoefu wa kuhimili presha ya Ligi Kuu.

Mwanaspoti limedokezwa, Kigonya anafanya mazungumzo na yamefikia hatua nzuri kwa ajili ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja aliowekewa mezani, huku uongozi wa kikosi hicho ukifanya siri kubwa kutokana na kutotaka kushindania na klabu nyingine.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota alisema wamekamilisha baadhi ya sajili kwa lengo la kuongezea nguvu kikosi hicho msimu ujao, hivyo watatangaza mmoja baada ya mwingine kwa muda muafaka.

Kipa huyo mbali na kuzichezea Azam na Yadah Stars, timu nyingine pia alizozichezea ni Tooro United FC na Bright Stars FC zote za kutoka kwao Uganda, Sofapaka FC na Kakamega Homeboyz za Kenya na Forest Rangers FC na Trident FC zote za Zambia.

Mbeya City iliyorejea tena Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, tayari imeanza mawindo ya nyota wa kuwaongezea nguvu, ambapo hadi sasa imekamilisha usajili wa aliyekuwa beki wa kati wa Mashujaa FC, Ibrahim Ame.