Mmoja afariki dunia, wengine kadhaa wakijeruhiwa ajali ya magari matano Mbeya

Mbeya. Mteremko wa Nzovwe jijini Mbeya umeendelea kugharimu maisha ya watu baada ya leo Jumapili, Julai 27, 2025 kuua mmoja na kujeruhi wengine kadhaa kufuatia ajali iliyohusisha magari matano na bajaji moja.

Ajali hiyo imetokea katika mteremko huo ambapo gari aina ya Lori ‘Howo’ kufeli breki na kuyagonga magari mengine manne yakiwamo ya abiria na bajaji moja.

Ajali hiyo imekuwa mwendelezo katika mteremko huo unaohusisha maeneo ya Simike, Mbembela na Iyunga ambapo mara ya mwisho kutokea ajali kubwa iliua watu 13 na kujeruhi 18, Juni 5,2024.

Ofisa Operesheni wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, Gervas Fungamali amesema baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo wamefika kwa ajili ya kuokoa jambo ambalo wamefanikiwa.

Amesema kwa taarifa za awali, mtu mmoja ambaye jina lake halikujulikana haraka amefariki dunia ambaye alikuwa kwenye bajaji.

“Ajali imetokea leo saa 11 jioni ambapo lori likiwa na shehena ya mbolea kutokea nchini Congo liligonga gari aina ya Rosa, Hice, Howo na Rosa kisha bajaji na kuua mmoja,” amesema.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Majeruhi bado hatujajua kwakuwa wamepelekwa Hospitali ya rufaa Mkoa wa Mbeya, hivyo baada ya kuwaona tutajua idadi kamili na maendeleo kwa ujumla,” Amesema Fungamali.

Mmoja wa abiria aliyekuwa katika Hice, Godfrey Mwanja amesema hawakuelewa kilichowakuta zaidi ya kujikuta wakitumbukia kwenye shimo.

“Binafsi sikujua kilichotokea ndio maana unaona nimeloa na kuchakaa nguo, nilijitambua nikiwa kwenye shimo ila nashukuru niko salama,” amesema Mwanja.

Naye Gozbert Msanya, mmoja wa mashuhuda amesema akiwa katika gari lake alishuhudia lori hilo likiyagonga magari mengine kuanzia Nzovwe hadi Iyunga na kwamba kwa macho yake aliona maiti moja.

“Mimi nilikuwa kwenye gari langu lori likatoka nyuma nikalipisha upande mmoja likawa linagonga gari moja moja hadi kule daraja la Iyunga ndipo likatumbukia chini, nimeona mtu mmoja akiwa amefariki,” amedai Msanya.

Endelea kufuatilia Mwananchi