Morogoro. Alex Thobias maarufu Sanchez (23) ameuawa kwa madai ya kupigwa risasi wakati akijaribu kuruka ukuta ili kuwatoroka polisi waliofika nyumbani kwake kumkamata.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 27, 2025 kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, kijana huyo, mkazi wa Mtaa wa Mahita, kata ya Chamwino, Manispaa ya Morogoro, alipigwa risasi wakati akiwakimbia polisi waliokwenda kumkamata.
Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kutokana na kutuhumiwa kwenye matukio ya unyang’anyi na wizi wa pikipiki katika maeneo tofauti mkoani Morogoro.
Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa huyo, Julai 26, 2025 asubuhi, alikuwa amejificha kwa mpenzi wake anayeishi Chamwino baada ya kuiba pikipiki eneo la Msamvu, usiku wa kuamkia Julai 25, 2025 na kutoweka nayo.
“Taarifa za tukio hilo la wizi wa pikipiki zilifikishwa polisi, askari waliokuwa doria wakishirikiana na wananchi wema walifanikiwa kumpata mtuhumiwa akiwa na pikipiki hiyo nyumbani kwa mpenzi wake (jina limehifadhiwa),” amesema Kamanda Mkama.
Amesema baada ya kuhisi amezingirwa na polisi, mtuhumiwa aliamua kuruka ukuta wa uzio wa nyumba aliyokuwa amejificha kwa lengo la kuwatoroka askari waliokuwa wamejihami kwa silaha.
Hata hivyo, amesema katika harakati za kumkamata mtuhumiwa huyo, alijeruhiwa kwa risasi mguuni na kukamatwa.
Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa huyo alifikishwa hospitali na kubainika amefariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.

Polisi wamejaribu kuisoftisha hii taarifa badala ya kusema moja Kwa moja wamehusika kumpiga risasi huyu mtuhumiwa
Hata hivyo, Kamanda Mkama amewataka vijana kufanya kazi zilizokuwa halali ili wajipatie kipato badala ya kujiingiza kwenye matukio ya wizi na mengine ya kihalifu.
Baadhi ya madereva wa bodaboda wametoa maoni tofauti kufuatia tukio hilo hasa kutokana kukithiri kwa matukio ya uporaji wa pikipiki.
Akizungumzia tukio hilo, Shabani Idd ambaye ni dereva wa bodaboda Stendi ya Msamvu, amesema bado kuna mtandao wa wezi wa pikipiki.
“Wezi wa aina hii hapa mjini wapo wengi na wanamtandao wao, wanajua wapi pa kuiba, wapi pa kuficha na wapi pa kuuzia. Polisi wasipofanikiwa kukamata huu mtandao, siku si nyingi pikipiki nyingine zitaendelea kuibwa,” amesema.
Bodaboda mwingine kutoka kijiwe cha Masika, Mussa Salumu amesema, “kitendo cha kuwakamata na kuwapeleka polisi peke yake hakitoshi kumaliza wizi wa pikipiki hapa mjini, dawa ni kuwakamata na kuwafunga vifungo vikubwa, ikitokea mwizi wa pikipiki siku anafungwa miaka 15 au 20, hakuna kijana atakayethubutu kuiba, lakini hili suala la kuwakamata siku mbili anatoka kwa dhamana, ndio maana wizi unashamili.”