Ni wakati wa wanaume kuwa wanaume halisi

Katika jamii nyingi duniani, hususan zile za Kiafrika, nafasi ya mwanaume katika familia imekuwa ikichukuliwa kuwa ya uongozi, ulinzi na uangalizi.

Hii haimaanishi kuwa mwanamke hana wajibu wala mchango, bali inaweka bayana kuwa mwanaume ana wajibu mkubwa wa kuhakikisha ustawi wa mwanamke wake kwa hali zote kiuchumi, kihisia, na kijamii.

Leo acha nitumie uwanja huu kuzungumza na wanaume ambao wamesahau jukumu lao la kuwatunza wanawake zao, mambo haya ndiyo yanasababisha ndoa na mahusiano ya watu kuingia kwenye migogoro.

Huko mitandaoni habari ya mjini ni sasampa, sitaki kujikita sana huko kwa sababu hata ukiniambia ipi ni maana halisi ya huo msamiati sitakuwa na majibu ila ninachoona ni mtu ameamua kuutumia kupeleka ujumbe wake kwa wanaume akiwakumbusha kuwahudumia wenza wao.

Kwa kuwa hili limekuwa tatizo kubwa ndiyo maana mjadala huo umebebwa na wanawake, wakilalamika wanaume wa sasa wamekuwa wagumu kutimiza majukumu yao.

“Sasa kama huna hutaki kuhudumia unataka uwe na mwanamke wa nini, wanaume wa siku hizi wanapenda ganda la ndizi,” alisema mwanamke mmoja kwenye mjadala.

Nikaona leo uwanjani niwakumbushe kaka zangu kwamba kumhudumia mwanamke si tu ni ishara ya mapenzi, bali pia ni wajibu wa kimaadili na kijamii unaochangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha familia na jamii kwa ujumla.

Mwanamke anapokuwa katika uhusiano au ndoa, hutoa muda wake, nguvu, na mara nyingi hujitolea kwa ajili ya ustawi wa mwanaume na familia kwa ujumla.

Anapopokea huduma na upendo kutoka kwa mwanaume, hujiona anathaminiwa, jambo ambalo huimarisha uhusiano kati yao na kuongeza mshikamano wa familia.

Mwanamke anapohudumiwa huweza kutimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Mfano, anapopewa msaada wa kifedha au kihisia, huondokana na msongo wa mawazo na hivyo kumwezesha kulea watoto vizuri, kuendesha shughuli za kijamii, au hata kujishughulisha na kazi za kujitegemea.

Mwanamke mwenye amani ya moyo na anayejua kuwa anajaliwa, huwa na nguvu ya kutoa mapenzi ya kweli na kujitolea kwa familia.

Ukweli ni kwamba jamii humheshimu mwanaume anayejali na kumthamini mpenzi au mke wake. Anaonekana kuwa ni kiongozi mwenye busara, mwenye utu na anayejua maana ya familia.

Kinyume chake, mwanaume asiyejali familia yake mara nyingi huonekana kuwa dhaifu kimaadili na hukosa heshima miongoni mwa wanajamii.

Familia ni msingi wa taifa lolote hivyo ikiwa kila mwanaume atamthamini na kumhudumia mwanamke wake, basi familia zitajengwa juu ya misingi ya upendo, mshikamano na kuheshimiana.

Watoto watakaozaliwa katika familia hizo watakua wakijifunza kuhusu wajibu wa kila jinsia na umuhimu wa kusaidiana, jambo litakalosaidia kujenga jamii yenye maadili.

Katika uhusiano wenye usawa, kila mmoja anapaswa kuchangia ustawi wa mwenzake. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali, mwanamke mara nyingi hujikuta akiwa na mzigo mkubwa wa majukumu.

Hivyo basi, ni wajibu wa mwanaume kuhakikisha anamsaidia kwa hali na mali ili kuhakikisha uhusiano unaendelea kuwa na afya na tija.

Ni ukweli usiopingika kwamba kumhudumia mwanamke ni jukumu la msingi la mwanaume ambalo lina faida si tu kwa uhusiano wao wa karibu, bali pia kwa familia na jamii kwa ujumla.

Hii ni njia ya kujenga uhusiano wa kweli unayojengwa juu ya msingi wa heshima, upendo na msaada wa dhati.

Ni wajibu wa kila mwanaume kujiuliza, je, anamhudumia vema mwanamke wake? Kama jibu ni la, basi ni wakati wa kubadili mtazamo na kuchukua hatua sahihi.