Sifa nne beki mpya Simba

WAKATI mashabiki wa Simba SC wakifurahia taarifa za usajili wa beki wa kimataifa wa Afrika Kusini, Rushine De Reuck, mmoja wa wapinzani wake wa muda mrefu katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Qobolwakhe Sibande, ametia neno kuhusu ubora wake huku akitaja mambo manne aliyonayo.

Sibande anayekipiga klabu ya TS Galaxy, aliwahi kukutana na De Reuck mara kadhaa katika mechi za ushindani wa ndani huko Afrika Kusini, na hakusita kueleza kuhusu ubora wa mchezaji huyo aliyewahi kutikisa akiwa na Maritzburg United kabla ya kutua Mamelodi Sundowns ambayo aliitumikia kwa miaka minne akisema ni mzuri katika kusoma mchezo kwa haraka, mtulivu, mgumu kupitika na kiongozi uwanjani hata kama sio nahodha.

“Rushine ni mchezaji aliyepevuka. Kitu cha kwanza kutoka kwake ni namna anavyoweza kusoma mchezo kwa haraka. Yaani kabla hata hujafanya kitu, yeye tayari anajua utakachofanya. Ana akili kubwa ya soka,” alisema Sibande.

Katika soka la kisasa, uwezo wa kuongoza safu ya ulinzi bila kupaniki ni jambo linalotafutwa na makocha wengi, Sibande alisema De Reuck ana sifa hiyo kwa asilimia kubwa.

“Anacheza kwa utulivu mkubwa, anajua wapi pa kusimama, na anafanya maamuzi sahihi hata timu inapokuwa kwenye presha kubwa.

“Ukicheza dhidi ya De Reuck, unakutana na ukuta uliojengwa kwa akili. Siyo beki wa kukimbizana tu na washambuliaji, bali anakuzuia kwa nidhamu. Anakupa presha ya kimyakimya lakini yenye matokeo makubwa. Anaongoza timu kama nahodha wa ulinzi, hata kama hajavaa kitambaa,” alisema.

Simba imeripotiwa kumsajili De Reuck kwa mkataba wa mwaka mmoja, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mwingine endapo atatimiza matarajio ya benchi la ufundi.

Kati ya mafanikio ya De Reuck akiwa na Mamelodi Sundowns ni pamoja na kushinda mataji saba ndani ya miaka minne, ikiwa ni pamoja na mataji manne ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL).

Sibande, ambaye aliwahi pia kucheza dhidi ya Yanga SC katika mashindano ya Kombe la Toyota mwanzoni mwa msimu uliopita, alisema ameona kiwango cha soka la Tanzania na anajua aina ya wachezaji wanaoweza kufanya vizuri.

Anaamini De Reuck anaweza kuwa chachu ya mafanikio kwa Simba kama atachezeshwa kwa uhuru na kupewa nafasi ya kuongoza.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Kocha Fadlu Davids, kufanya kazi na beki huyo ambaye ametoka kuitumikia Maccabi Petah Tikva ya Israel kwa mkopo, wawili hao walifanya kazi kwa mara ya kwanza wakiwa Maritzburg United ya Afrika Kusini.