Katika dunia ya sasa ambapo simu janja hazituachi mikononi mwetu, si jambo la kushangaza kuwa hata mapenzi sasa yamehamia mtandaoni.
Programu na mitandao ya kutafuta wachumba imebadilisha kabisa namna watu wanavyokutana, kuwasiliana na hata kupendana.
Enzi za kukutana kupitia kwa marafiki, shuleni, kazini au kwa bahati tu barabarani, sasa zinaanza kupotea. Leo unaweza tu kuingia mtandaoni ukabofya kitu au kutumia ujumbe, kitendo hicho kikatosha kuanza safari mpya ya kiuhusiano.
Miaka ya 2000 ilipoibuka mitandao ya kutafuta wachumba, wengi waliona kama ni njia ya mwisho kwa waliokata tamaa.
Lakini hadi kufikia mwaka 2025, programu hizi zimekuwa maarufu na ni sehemu ya kawaida ya maisha ya watu. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 300 duniani wanatumia programu za kutafuta wachumba, huku karibu asilimia 40 ya wapenzi wakisema walikutana mtandaoni.
Sababu kubwa ya kupanda kwa umaarufu wa mapenzi ya kidijitali ni urahisi wake. Ratiba za kazi zilizobana, kuhama kutoka miji hadi miji, na utegemezi mkubwa wa teknolojia vimewafanya watu wawe na nafasi ndogo ya kukutana ana kwa ana.
Programu hizi hufupisha muda wa kutafuta mchumba kwa kutumia vigezo mbalimbali kama umri, maslahi, thamani za maisha, hadi alama za nyota.
Programu kama ‘Hinge’ zinajitangaza kuwa “zimeundwa ili zifutwe” — zikisisitiza uhusiano wa kudumu badala ya uhusiano wa muda mfupi.
Program ya ‘Bumble’ kwa upande wake huwapa wanawake nafasi ya kuchukua hatua ya kwanza, jambo linaloendana na mabadiliko ya kijamii kuhusu nafasi za kijinsia katika mapenzi.
Ingawa programu hizi huongeza nafasi ya kukutana na watu wapya, changamoto pia zimeongezeka. Moja ya matatizo yanayojitokeza ni kile kijulikanacho kama “ghosting” yaani mtu kuacha kuwasiliana ghafla bila maelezo.
Wengine huchukulia programu hizi kama michezo tu ya kuburudisha bila nia ya kweli, jambo linalokatisha tamaa wanaotafuta uhusiano wa maana.
Zaidi ya hapo, kuna suala la uhalisia. Picha za wachumba huwa zimehaririwa kwa kuongeza mvuto zaidi kwa wahusika, huku hali ikiwa ni tofauti kiuhalisia pale wanapokutana uso kwa uso.
Aliyeonekana mrembo na kijana kwenye picha, kwa mshangao huja onekana kama kituko. Umri kumbe umesogea na hana tena mvuto kwa yule aliyemtamani. Watu hufikia hatua ya kuchanganyikiwa wanapojua uhalisia wa wenza wao baada ya kuonana uso kwa uso.
Licha ya changamoto, wapo waliopata furaha kupitia programu hizi. Joyce Tumali na Adam Kusekwa wote vijana wa miaka 30, walikutana kupitia mitandao ya Hinge wakati wa janga la Uviko-19.
“Tuliongea sana kabla ya kukutana,” anasema Joyce na kuongeza: “Ilipofika siku ya kukutana tulihisi kama tunajuana kwa muda mrefu.” Sasa wawili hao wameoana na wanakiri kuwa programu hiyo iliwaleta pamoja.
Mustakabali wa uhusiano wa kimtandao
Teknolojia inaendelea kukua, vivyo hivyo kwa mapenzi ya kidijitali. Kuna programu zinazojaribu kuunganisha watu kupitia video za utambulisho, sauti, au hata kutumia ukweli halisi kwa ajili ya miadi ya mtandaoni.
Lakini pamoja na hayo yote, hitaji la msingi halijabadilika: kutafuta mtu wa kuelewana, kupendana, na kushirikiana maisha. Iwe kwa njia ya mtandao au mkutano wa ana kwa ana, hamu ya mapenzi ya kweli bado inatawala.
Ni wazi kuwa programu za kutafuta wachumba zimeleta mageuzi makubwa katika namna watu wanavyopendana na kuanzisha uhusiano.
Japokuwa kuna changamoto, pia kuna fursa za kipekee ambazo hazikuwapo awali. Mapenzi ya kidijitali huenda si kamilifu, lakini ni halisi na yapo na ni jambo linaloendelea kustawi kila siku.
Mkazi wa jijini Mwanza, Anastazia James anasema siku moja katika kupitia mitandao, aliona picha ya mwanafunzi aliyesoma naye sekondari.
‘’Nilivutiwa na sura yake na maneno mazuri aliyokuwa akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook. Nikajikuta nikiingia kwenye profile yake (wasifu wake) mara kwa mara hadi nikajikuta namtumia ombi la urafiki. Ilichukua zaidi ya mwezi hadi alipolikubali. Kwa kipindi hicho nilikuwa nimeachana na mchumba wangu, nilihisi mpweke na mwenye maumivu ya moyo. Nilihitaji mtu wa kuzungumza naye hata kwa ujumbe tu,’’ anasema na kuongeza:
‘’Nilianza kumwandikia kwenye inbox yake ya facebook, nilituma ujumbe bila majibu hadi siku moja alipojibu. Tukaanza kuchati na baadaye tukabadilishana namba. Maongezi yakawa ya kila siku, tukaanza kupigiana simu na hata video call. Kadri muda ulivyozidi kwenda, hisia zikakua. Siku moja tulipanga na kukutana uso kwa uso na tukaanzisha uhusiano wa kimapenzi rasmi.
Anaongeza: “Nilidhani ni wa muda tu, lakini moyo wangu ukazidi kuvutwa kwake. Siku haikupita bila kuwasiliana, tulizidi kuonana mara kwa mara. Baada ya miezi sita tangu tumefahamiana mwaka 2016 hatimaye tukafunga ndoa na sasa tuna watoto wawili.’’