Dar es Salaam. Wajasiriamali vijana wa Kitanzania wametakiwa kuona umuhimu wa kusajili biashara ili kuleta ushindani kwa ngazi ya kimataifa na kufanya shughuli zao kwa weledi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga katika mkutano wa wajasiriamali wa Afrika-Asia ulioanza Ijumaa na kufikia tamati leo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku takribani wajumbe 750 wakishiriki.
Ulanga amesema mkutano huo ni jukwaa la kipekee kwa wajasiriamali vijana kuunganishwa na fursa na wawekezaji kwa kuwa unaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania na mwelekeo wa uchumi wa dunia.
Mkutano huo ulioandaliwa na Chama cha Wawekezaji Vijana na Mediaprenuer Nigeria/India, unafungua macho kwa vijana wa Kitanzania kuwa na ndoto ya ushindani kwa ngazi ya kimataifa na kujaribu kufanya kile ambacho vijana wa nchi nyingine wanakifanya.
“Vijana ndio rasilimali yenye nguvu zaidi Tanzania. Lakini, mara nyingi, tunaona uwezo ambao haujatumika. Mataifa mengine yamethibitisha kwamba, vijana wakiwezeshwa, uchumi unastawi. Hatuwezi kumudu kubaki nyuma, huku wengine wakienda mbele. Tukishindwa kuwatumia vijana wetu leo, tuna hatari ya kupoteza kizazi cha wabunifu, na viongozi,” amesisitiza Ulanga.
Mkurugenzi huyo amewahakikishia wajumbe kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Nigeria, China, Ghana, India na Marekani kwamba, Serikali ya Tanzania inafanya kazi bila kuchoka ili kurahisisha michakato ya biashara na uwekezaji, kupunguza vikwazo na kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali.
“Jukumu lenu ni kuandaa na kuweka biashara zenu katika nafasi ya kutumia fursa hizi,” amesema Ulanga.
Amesisitiza kwamba, ikiwa Tanzania inataka kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, haiwezi kuridhishwa na biashara ndogo ndogo zisizo rasmi, huku akisisitiza haja ya kujiinua, kurasimisha na kufanya kazi kiweledi.
Amewashauri vijana kuhakikisha wanarasimisha biashara zao mapema kwa kuzisajili, kuweka kumbukumbu sahihi na kuzingatia viwango na kutumia teknolojia ya kidijitali.
Pia, amesema wanapaswa wawe na chapa za biashara mtandaoni, wazingatia ubora na kuongeza thamani, watengeneze bidhaa zilizokamilika zinazoweza kushindana kimataifa, kujenga mitandao na ubia na kuendelea kuwa imara na kubadilika kulingana na mazingira.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalumu za Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Balozi Aziz Mlima amewataka vijana kuhakikisha wanajiandikisha Tiseza ili kutafiti fursa zilizopo za uwekezaji.
“Nawasihi mrahisishe biashara ili kupata msaada wa Tiseza na mipango mingine ya uwekezaji ya kitaifa kwa kuwa mazingira ya sasa ya uchumi wa Tanzania yamewekwa kuwavutia wawekezaji wa ndani na wa nje,” amesema.