Dar es Salaam. Wakazi wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam wametakiwa kuacha matumizi holela ya bidhaa za plastiki, kwani yanahatarisha maisha ya viumbe hai na mazingira kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Julai 27, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule wakati wa shughuli ya usafi iliyofanyika katika eneo la Kunduchi Beach kwa lengo la kuhamasisha usafi wa mazingira.
Amesema matumizi ya plastiki yamekuwa tatizo kubwa, hususan mifuko na chupa za plastiki ambazo huishia baharini na kuathiri vyanzo vya maji, jambo linaloweza kusababisha athari kwa binadamu na viumbe wengine.
Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi wa Kinondoni kubadilisha tabia zao ili kulinda mazingira huku akisisitiza kuwa hali hiyo inahitaji ushirikiano wa kila mtu ili kufanikisha mabadiliko ya kweli.
“Sisi tumekuwa maadui wa uchumi wetu, tumekuwa maadui wa mazingira yetu, tumekuwa maadui wa baharini yetu na hivyo tunajiangamiza sisi wenyewe,” amesema Mtambule.
Ameongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja kutunza mazingira na kupunguza uchafuzi. Bila jitihada za pamoja, amesema athari za uchafuzi wa mazingira zitaendelea kudhoofisha uchumi na maisha ya binadamu na wanyama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Uvuvi wa Manispaa ya Kinondoni, Kulwa Mkwama amesisitiza kuwa ingawa jitihada za wadau wa mazingira ni kubwa, bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira hasa ya baharini.
Amesema plastiki nyingi bado hutupwa ovyo na huishia kuharibu mazingira ya bahari pamoja na mazalia ya samaki.
“Kiukweli mazingira yetu ya bahari hayapo vizuri, plastiki ni nyingi na uelewa wa wananchi katika kutunza mazingira ni mdogo,” amesema Mkwama akiongeza kuwa Manispaa ya Kinondoni itaendelea kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Soko la Samaki la Kunduchi Beach, Zed Mwinyi Zed ameeleza furaha yake kwa kuona soko lao likifanyiwa usafi kwani biashara ya samaki inategemea sana mazingira safi na yenye afya.
“Nimefurahi kuona usafi ukiendelea kufanyika hapa, kwani biashara yetu inahitaji mazingira safi. Naomba wananchi wa Kunduchi, hata baada ya wageni kuondoka, tuendelee kushirikiana kwa kufanya usafi sokoni hapa,” amesema Zed.
Mmoja wa wachuuzi katika soko hilo, Salumu Mikindo ameeleza changamoto wanazokutana nazo kuwa wengi wa wachafuzi wa mazingira ni wale wanaoishi juu ya maeneo ya milimani na siyo wale wanaoishi mabondeni.
“Watu wanadhani sisi ndio wachafu, lakini ukweli ni kwamba uchafu wote unaozalishwa huko juu huishia huku bondeni, hivyo tunaomba taasisi ziendelee kutusaidia,” amesema Mikindo.