Hai. Watu wasiojulikana wamevamia shamba la mwalimu mstaafu, Germana Mushi na kuharibu miundombinu ya kilimo ikiwemo mfumo wa umwagiliaji na mitambo ya sola, uharibifu unaokadiriwa kufikia zaidi ya Sh40 milioni.
Shamba hilo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 30, liko katika Kijiji cha Mkalama, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambapo zimeibiwa pampu za umwagiliaji, mfumo wa sola na kuchomwa moto mipira ya usambazaji maji shambani.
Tukio hilo limetokea Julai 19, 2025 wakati walinzi wa shamba hilo walipoondoka kwa dharura, mbali na kuiba mitambo ya umwagiliaji, walikata nyaya za mfumo wa sola na kuchoma mipira ya umwagiliaji na gari lililokuwa shambani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Taarifa za tukio hilo tunazo na tunaendelea kufuatilia kujua ni nani kafanya hivyo. Tunataka tujue kama ni mgogoro wa ardhi au ni wafugaji waliokuwa wakikamatwa. Kwa hiyo, uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo,” amesema Kamanda Maigwa.

Mwalimu mstaafu Germana Mushi akielezea uharibifu uliofanyika Shambani kwake
Akielezea tukio hilo, Mushi amesema mradi huo wa shamba waliuanzisha mwaka 2011 na mume wake wakiwa bado kazini, kwa nia ya kujenga msingi wa maisha baada ya kustaafu na pia kuwasaidia watoto wao waliomaliza vyuo vikuu lakini hawajapata ajira.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mushi, tukio hilo limeyumbisha ndoto ya familia yake ya kujitegemea kiuchumi, ndoto waliyoianza mwaka 2011 wakiamini shamba hilo lingeendelea kuisaidia familia hata baada ya kustaafu.
“Tulianzisha mradi huu kwa nguvu na matumaini na baada ya kustaafu, tuliamini ungekuwa mkombozi wetu kiuchumi. Lakini sasa, tumerudishwa nyuma. Pampu na inverter vimeibiwa lakini mipira ya umwagiliaji na gari lililokuwa shambani hapa, vimechomwa moto, ni uharibifu mkubwa,” amesema.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mushi, waliokuwa wakiangalia shamba hilo waliondoka na ndipo wavamizi walipotumia nafasi hiyo kuingia na kufanya uharibifu huo.
Peter Kiria, mmoja wa wanafamilia, amesema walipata taarifa za uharibifu huo Julai 19, 2025 na walifika shambani na kukuta hali ya kusikitisha.
“Tulipofika shambani tulikuta baadhi ya mali zikiwa zimechomwa moto, nyingine zimeibiwa na migomba kuharibiwa na mifugo. Ni tukio la kusikitisha. Tulitoa taarifa polisi na tumewaachia mamlaka kufuatilia. Tunatarajia Serikali itusaidie kupata haki na kuwabaini wahusika,” amesema Kiria.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkalama, Said Michael
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkalama, Said Michael amesema alipokea taarifa na alifika eneo la tukio, akashuhudia uharibifu mkubwa, ikiwemo kuchomwa kwa mipira ya umwagiliaji na kuharibiwa kwa mfumo wa sola.
“Tulifanya uchunguzi wa awali na kugundua huenda wafugaji ndio waliovamia kutokana na kuwepo kwa majani ya mahindi pale shambani, tumewaachia polisi wanaendelea na uchunguzi,” amesema mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kilimamswaki, John Onesmo amesema tukio hilo limeibua maswali mengi, hasa kitendo cha kuchoma mali ambacho kinaashiria huenda kuna sababu zaidi ya wizi wa kawaida.
“Kuiba ni moja, lakini kuchoma mali za mtu ni kitendo kinachostahili uchunguzi wa kina. Pia, kuna suala la mifugo kuingizwa shambani na vijana waliowahi kuonywa kabla, sasa hatujui kama kuna uhusiano wowote,” amesema.
Familia ya Mwalimu Mushi sasa inatoa wito kwa wadau wa maendeleo, taasisi za kifedha na Serikali kwa ujumla kusaidia kurejesha hali ya mradi huo ili ndoto yao ya kujikwamua kiuchumi na kusaidia jamii unayowazunguka itimie.