‘Watafiti shirikianeni na Serikali kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia’

Dar es Salaam. Watafiti wa masuala ya nishati safi ya kupikia wametakiwa kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati hiyo.

Wito huo umetolewa na Kamishna Msaidizi, Utafiti na Uundaji wa Miundo ya Kifedha kutoka Wizara ya Fedha, Dk Remidius Ruhinduka wakati wa kikao na watafiti kutoka Taasisi ya Inclusive Green Economy (IGE) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akizungumza kwenye kikao hicho jana Julai 26, 2025, Dk Ruhinduka amesema ushirikiano huo utaiwezesha Serikali kufanya uamuzi sahihi unaozingatia ushahidi wa kisayansi.

“Wakati tunatekeleza mkakati huu, kuna mambo mengi ndani ya Serikali yanayojulikana kwa kiwango kidogo. Tafiti zina nafasi kubwa katika kutoa mwanga. Tunapokuwa na watafiti ambao kazi yao wakiamka na kulala ni kutafuta majibu, basi lazima tufanye kazi kwa pamoja,” amesema Dk Ruhinduka.

Ameongeza kuwa, Serikali inahitaji watafiti hao kwa sababu wao ni Watanzania wanaotaka kuona nchi yao inapiga hatua. Pia, aliipongeza taasisi ya IGE kwa kuihusisha Serikali moja kwa moja katika tafiti zao, jambo alilosema linasaidia kupunguza upinzani wa kisera wakati wa utekelezaji.

Mkuu wa Mradi wa IGE-Lead, Dk Aloyce Heplwa amesema taasisi hiyo imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa watunga sera na kuwahusisha moja kwa moja katika tafiti ili kuimarisha utekelezaji wa sera.

“Mtafiti anaweza kuwa na kitu kizuri lakini mtunga sera hakifahamu. Sisi tumekuja kuwaunganisha hawa wawili. Tunataka wakati utafiti unafanyika, watunga sera washirikishwe mapema ili kuwe na ufanisi,” amesema Dk Heplwa.

Ameongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa sera nyingi za nishati safi, bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho ili kuleta manufaa kwa wananchi. Alieleza kuwa, Serikali inazalisha umeme wa kutosha lakini bado Watanzania wengi wanategemea kuni na mkaa kwa kupikia.

Mtaalamu wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, James Chuya, amesisitiza kuwa, matumizi ya nishati safi yana mchango mkubwa katika kuboresha afya za wananchi na kuimarisha uchumi wa Taifa.

“Bado idadi kubwa ya wananchi hawajui umuhimu wa kutumia nishati safi. Matumizi haya ni muhimu si tu kwa mazingira, bali pia kwa afya ya jamii yetu,” amesema Chuya.

Ameitaka Serikali kushirikiana na taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kutumia nishati safi, akisema bila kufanya hivyo, malengo ya kitaifa ya maendeleo endelevu hayatofikiwa.