Watakiwa kutunza mikoko kukabili mabadiliko tabianchi

Unguja. Wakati maeneo zaidi ya 120 ya kilimo yakiathirika kwa kuingiliwa na maji ya chumvi visiwani Zanzibar kutokana na ukataji wa mikoko usiozingatia matumizi endelevu, jamii imehamasishwa kutunza mikoko ili kuondokana na athari zinazojitokeza ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamebainishwa leo Julai 27, 2025 na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu, Said Juma Ali wakati akizungumza na wananchi wa Fujoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja katika shughuli ya upandaji wa mikoko ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Siku ya Mikoko Duniani.

“Hali hii inatishia maisha ya wakulima na wavuvi, hivyo natoa wito kwa jamii kuchukua hatua za haraka kulinda mikoko iliyopo kabla hatujaathirika zaidi,” amesema Ali. 

Mkurugenzi huyo ameitaka jamii kuacha tabia ya ukataji wa mikoko kwa matumizi yasiyo sahihi na badala yake washirikiane na taasisi husika katika juhudi za kuhifadhi na kudhibiti upotevu wa miti hiyo adimu.

Ofisa Mrejeshaji wa Mikoko kutoka Shirika la Mwambao (Coastal Community Network), Suleiman Mohamed Salim ameeleza kuwa kila mwaka katika maadhimisho ya siku ya mikoko, shirika hilo huungana na Serikali kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa mikoko.

Amesema wamekuwa wakifundisha namna ya kuchagua aina sahihi za mikoko kwa maeneo yaliyoathirika na kuhakikisha urejeshwaji katika hali yake ya asili unafanyika.

Asha Juma Ashkina amesema licha ya juhudi zilizopo bado kuna changamoto za uvamizi na ukataji wa mikoko, hali inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira. Ameiomba jamii kuacha ukataji wa miti ovyo na kushiriki kuhifadhi mazingira ya mikoko.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Ali Khamis Juma amezindua kitabu kipya kinachoitwa “Mangroves of Pemba” ambacho kinaelezea aina mbalimbali za mikoko, lengo likiwa ni kuongeza uelewa na kuhamasisha utunzaji wake.

Katibu huyo amesema jamii bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uelewa juu ya umuhimu wa mikoko, hali inayosababisha baadhi kuikata kwa ajili ya kujikimu kimaisha. 

Katika maadhimisho hayo, miche 6,500 ya mikoko aina ya magondi, mchu na mkandaa mwekundu ilipandwa katika maeneo manne ya Zanzibar Fujoni na Tumbatu kwa upande wa Unguja, na Shidi pamoja na Mtangani kwa upande wa Pemba.