WATU WASIOJULIKANA WADAIWA KUTEKETEZA NA KUHARIBU MALI ZENYE THAMANI YA MILIONI 40..

Na WILLIUM PAUL, HAI. 

WATU wasiojulikana wanatuhumiwa kuvamia shamba la mwalimu mstaafu Germana Mushi na kuharibu miundombinu muhimu ya kilimo, likiwemo mfumo wa umwagiliaji na mitambo ya sola, uharibifu unaokadiriwa kufikia zaidi ya Sh milioni 40.

Shamba hilo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 30, liko katika kijiji cha Mkalama Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro ambapo uharibifu uliofanyika ni pamoja na wizi wa pampu za umwagiliaji, mfumo wa sola na mipira.

Tukio hilo lilitokea Julai 19, 2025 wakati walinzi wa shamba hilo walipoondoka kwa dharura ambapo watu hao waliovamia mbali na kuiba mitambo ya umwagiliaji, walikata waya za mfumo wa sola na kuchoma mipira ya umwagiliaji na gari lililokuwa shambani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

“Taarifa za tukio hilo tunazo na tunaendelea kufuatilia kujua ni nani kafanya hivyo. Tunataka tujue kama ni mgogoro wa ardhi au ni wafugaji waliokuwa wakikamatwa. Kwa hiyo uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo” alisema Kamanda Maigwa.

Akielezea tukio hilo, Mushi alisema  mradi huo wa shamba waliuanzisha mwaka 2011 na mume wake wakiwa bado kazini, kwa nia ya kujenga msingi wa maisha baada ya kustaafu, na pia kuwasaidia watoto wao waliomaliza vyuo vikuu lakini hawajapata ajira.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mushi, tukio hilo limeyumbisha ndoto ya familia yake ya kujitegemea kiuchumi, ndoto waliyoianza mwaka 2011wakiamini shamba hilo lingeendelea kuisaidia familia hata baada ya kustaafu.

“Tulianzisha mradi huu kwa nguvu na matumaini na baada ya kustaafu, tuliamini ungekuwa mkombozi wetu kiuchumi. Lakini sasa, tumerudishwa nyuma. Pampu na inverter vimeibiwa lakini  mipira ya umwagiliaji na gari lililokuwa shambani hapa  vimechomwa moto, ni uharibifu mkubwa,” alisema kwa huzuni.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mushi, waliokuwa wakiangalia shamba hilo walikuwa wameondoka na ndipo wavamizi walipochukua fursa hiyo kuingia na kufanya uharibifu mkubwa katika eneo hilo. 

Alisema mradi huo wa shamba alianzishwa na marehemu mume wake  na uwekezaji waliouweka hapo hadi sasa unakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh 200 Milioni 

Peter Kiria, mmoja wa wanafamilia, alisema walipata taarifa za uharibifu huo siku ya Jumamosi Julai 19,2025 na walifika shambani na kukuta hali ya kusikitisha.

“Tulipofika shambani tulikuta mali zikiwa zimechomwa moto, baadhi zimeibiwa, na migomba kuharibiwa na mifugo. Ni tukio la kusikitisha. Tulitoa taarifa polisi na tumewaachia mamlaka kufuatilia. Tunatarajia serikali itusaidie kupata haki na kuwabaini wahusika,” alisema Kiria.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkalama, Said Michael alisema alipokea taarifa za tukio hilo na alifika eneo la tukio, akashuhudia uharibifu mkubwa, ikiwemo kuchomwa kwa mipira ya umwagiliaji na kuharibiwa kwa mfumo wa sola.

 “Tulifanya uchunguzi wa awali na kugundua huenda wafugaji ndio waliovamia, kutokana na kuwepo kwa majani ya mahindi pale shambani, tumewaachia polisi wanaendelea na uchunguzi” amesema mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kilimamswaki, John Onesmo alisema tukio hilo limeibua maswali mengi, hasa kitendo cha kuchoma mali ambacho kinaashiria huenda kuna sababu zaidi ya wizi wa kawaida.

 “Kuiba ni moja, lakini kuchoma mali za mtu ni kitendo kinachostahili uchunguzi wa kina. Pia kuna suala la mifugo kuingizwa shambani na vijana waliowahi kuonywa kabla, sasa hatujui kama kuna uhusiano wowote,” amesema.

Familia ya Mwalimu Mushi sasa inatoa wito kwa wadau wa maendeleo, taasisi za kifedha na serikali kwa ujumla kusaidia kurejesha hali ya mradi huo ili ndoto yao ya kujikomboa kiuchumi na kusaidia jamii itimie.