12 zapeta Yamle Yamle Cup, 13 zikiaga

Baada ya kukamilika hatua ya makundi ya mashindano ya Yamle Yamle Cup, timu 12 zimefuzu hatua ya 12 bora upande wa kisiwani Unguja.

Timu ambazo zimefuzu ni Mazombi FC, Welezo City, Al Qaida FC, Mwembe Makumbi Combine, Melitano City, Nyamanzi City, Magari ya Mchanga, Real Nine City, Miembeni City, Melinne City, Kundemba FC na Kajengwa FC.

Kwa upande wa zilizoaga ni Manyalu FC, Mborimborini, Monduli Combine, Sokoni Kwerekwe, Kipungani, Wadachi FC, Pwani Mchangani, B5 FC, Mambosasa, Kinazini, Sokoni Kwerekwe, JKU Academy na Luxury FC.

Katika mashindano hayo, Mwembe Makumbi na Al Qaida zimeweka rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye mchezo mmoja ambapo Mwembe Makumbi ilishinda 10-0 dhidi ya Kinazini, huku Michael Joseph akifunga mabao sita peke yake. Nayo Al Qaida ilipata ushindi kama huo dhidi ya Mambosasa ambapo Matheo Anthony alifunga mabao saba peke yake.

Kwa mujibu wa waandaaji, timu zitakazofanikiwa kutinga hatua ya robo ya fainali ya mashindano hayo zitapatiwa Sh1 millioni kwa ajili ya maandalizi.

Bingwa wa mashindano hayo atabeba Sh20 millioni na medali za dhahabu, wa pili Sh10 millioni na medali za fedha, wa tatu Sh5 millioni na medali za shaba, huku wa nne Sh3 millioni.

Mfungaji bora ataondoka na bajaji na mfungaji bora kijana na kipa bora kila mmoja akizawadiwa pikipiki.

Timu yenye mashabiki bora wenye nidhamu itachukua Sh1 millioni na mfanyabiashara atakeyedumisha usafi viwanjani ataondoka na Sh1 millioni kutoka kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita.

Mashindano hayo kwa sasa yanaendelea kisiwani Pemba kwa kutafutwa timu nne zitakazoungana na 12 kukamilisha timu 16 zitakazoendelea kuchuana kuwania ubingwa wa mashindano hayo.