PACHA ya eneo la kiungo cha ukabaji ndani ya Yanga imevunjika kwa kuondoka mkongwe mmoja tu. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya timu hiyo kumuongezea mkataba wa miaka miwili Duke Abuya
Yanga eneo hilo la kiungo ilikuwa inaongozwa na Khalid Aucho, Mudathir Yahya na Abuya ambapo nyota hao watatu walikuwa mhimili mkubwa wa mafanikio ya klabu hiyo.
Kuelekea msimu ujao, Aucho hatakuwepo baada ya kumaliza mkataba wake na klabu hiyo kutangaza kutoendelea naye, huku Mudathir na Abuya kila mmoja akiongezewa mkataba wa miaka miwili baada ya wao pia muda wao kumalizika.
Wakati Aucho akiondoka, Yanga imemleta Moussa Balla Conte kutoka CS Sfaxien ya Tunisia akitajwa kuwa ndiyo mbadala wake.
“Ilikuwa ni lazima aongezwe mkataba mpya kutokana na ripoti ya benchi la ufundi lakini pia ubora aliouonyesha ni sehemu ya mafanikio tuliyoyapata msimu uliopita, tutaendelea kuwa naye na tunatarajia makubwa kutoka kwake,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
“Safu yetu ya kiungo ilikuwa bora sana, hatukuwa na makosa tukitumia nyota watatu wote wakigawana dakika, tumeshindwa kumshawishi Aucho ambaye ameamua kuondoka lakini tunaamini waliopo watasaidiana na usajili mpya kuifanya Yanga kuwa na muendelezo uleule wa ubora.”
Mbali na Duke, pia Yanga imemalizana na Maxi Nzengeli ambaye naye ameongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Tayari Maxi ameitumikia Yanga kwa misimu miwili na amekuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo akicheza mechi 100 kwa kipindi hicho akifunga mabao 26 kwenye mashindano yote, ametoa pasi 15 zilizozaa mabao na ametwaa mataji saba.
Nyota huyo alijiunga na Yanga 2023-2024 kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Union Maniema ya DR Congo ambapo msimu wake wa kwanza alifunga mabao 11, hakuwa na asisti.
Msimu uliopita 2024-2025 licha ya kusumbuliwa na majeraha muda mrefu, namba zake bado zimekuwa nzuri kwani amefunga mabao sita na kutoa pasi 10 zilizozaa mabao.